WAZIRI
Mkuu, Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
kupitia Jeshi la Polisi kufanya upelelezi kuwabaini waliohusika na
mauaji ya watu saba ambao miili yao iliokotwa pembezoni mwa mto Ruvu
wilayani Bagamoyo, mkoa wa Pwani, ikiwa kwenye mifuko ya sandarusi, ili
hatua kali zichukuliwe dhidi yao.
Waziri
Mkuu Majaliwa amesema serikali imepokea kwa huzuni kubwa taarifa ya
kuokotwa kwa miili hiyo Desemba 8, mwaka huu na kueleza kuwa matukio
kama hayo, likiwemo la mjasiriamali kuuawa baada ya kutekwa mkoani
Tabora, hayavumiliki wala kukubalika.
Alitoa
maagizo hayo jana katika Baraza la Maulid ya kuzaliwa Mtume Muhammad
(S.A.W) lililofanyika kitaifa kijijini Shelui wilayani Iramba mkoani
Singida. Waziri Mkuu Majaliwa alikuwa mgeni rasmi.
Alisema,
“Serikali kwa kushirikiana na Polisi, tena Waziri wa Mambo ya Ndani uko
hapa (akimzungumzia Mwigulu Nchemba aliyekuwepo katika baraza hilo),
tutaendelea na upelelezi ili wahusika wachukuliwe hatua kali.”
Jana
akihojiwa katika kituo cha televisheni cha Star TV, Mwigulu alisema
uchunguzi umebaini kuwa miili saba iliyookotwa Bagamoyo ni ya wahamiaji
haramu.
Miili
ya watu sita ilikutwa Desemba 7, mwaka huu kando ya mto Ruvu wilayani
Bagamoyo ndani ya mifuko ya sandarusi na ikiwa imewekwa mawe ili isielee
kisha mifuko hiyo kushonwa kama mzigo wa mazao na kutupwa mtoni.
Mwili
mwingine uliokotwa Desemba 9, eneo hilo hilo na pamoja na kutokuwa
katika mfuko wa sarandusi, ulikuwa umevuliwa shati na kuonekana na
majeraha mgongoni na kwenye ubavu umekatwa na kitu chenye ncha kali.
Mwishoni
mwa wiki, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Boniventure Mushongi alisema
miili yote ilizikwa kwa kuwa ilikuwa vigumu kuwatambua kutokana na
kuharibika vibaya huku kukiwa hakuna kitambulisho chochote
kinachoashiria watu hao ni nani na wametoka wapi na kwamba Polisi
inaendelea na upelelezi kubaini waliohusika na mauaji hayo na
atakayebainika sheria itachukua mkondo wake.
Aidha,
Waziri Mkuu alisema serikali ipo macho kukabiliana na tishio lolote la
usalama na vyombo vya usalama vipo tayari muda na wakati wote.
Aliwataka
wananchi kushirikiana na vyombo vya usalama kutoa taarifa wanapoona
kuna hatari kwani viongozi wa dini na waumini wa dini hizo ndio walinzi
wa Taifa.
Alisema
uwepo wa vikundi vya uhalifu kama ‘panya road’ cha jijini Dar es Salaam
ni hatari kwa jamii, kwani vinadhuru na kuvuruga amani na kueleza kuwa
ni vijana na watoto wanaoishi katika jamii, walioko misikitini na
makanisani na kutaka waripotiwe katika vyombo vya usalama ili
washughulikiwe.
Alizungumzia
ugaidi na kubambikizwa kesi, na kusema serikali itaendelea kusimamia
mtu kupata haki zake na anayestahili adhabu, kuipata vile vile.
“Ni heri kuwa na watu 10 waliotoroka mahabusu kuliko mtu mmoja kukaa mahabusu kwa kesi ya kuonewa,” alisema Majaliwa.
Mwigulu anena kuhusu miili 7, Saanane
Akizungumza
jana kwa simu kuhusu vifo hivyo vya Bagamoyo, Waziri wa Mambo ya Ndani
ya Nchi, Mwigulu Nchemba alisema serikali baada ya tukio hilo ilichukua
hatua kupitia vyombo vya usalama na tayari Mkuu wa Jeshi la Polisi
nchini, Inspekta Jenerali, Ernest Mangu amemhakikishia wanalifanyia
kazi.
“Kama
nilivyosema awali, hatujajua asilimia mia kwa mia kama watu hao
waliouawa wana connection (uhusiano) na wahamiaji haramu waliookotwa
wamechoka sana hivi karibuni (juzi).
“Kuna
wahamiaji 81 waliokotwa hawajitambui, wameishiwa nguvu kabisa, ni eneo
hilo hilo kulikookotwa miili hiyo, tumehisi watu waliowabeba wahamiaji
hao inawezekana wengine walikufa na kwa vile hawana utu, wakawafunga
katika viroba (sarandusi) na kuwatupa, Polisi wanachunguza hili kwa
kina,” alieleza Mwigulu.
Aidha, alisema pia Polisi inachunguza ikiwa miili hiyo ilitupwa kikatili na wasafirishaji wa binadamu ambao nao hawana utu.
Alipoulizwa
kwa nini wazikwe haraka bila vipimo vya vinasaba, Mwigulu alisema kuwa
alizungumza na IGP na kuelezwa kuwa miili hiyo ilikuwa katika hali mbaya
sana, lakini pia kuzikwa hakuzuii uchunguzi kufanyika kujua chanzo cha
vifo hivyo.
Kuhusu
kupotea katika mazingira ya kutatanisha Ofisa wa Ofisi ya Chadema,
Makao Makuu Dar es Salaam, Bernard Saanane Novemba 18, mwaka huu,
Mwigulu alisema aliona taarifa hizo kupitia mitandao ya kijamii na kwa
kuwa alikuwa akimfahamu, alimpigia simu na kubaini simu haipatikani.
“Nilishtuka
kuona hizi habari, binafsi ni rafiki yangu wa karibu, nilipoona hizi
habari nilimpigia na sikumpata, baada ya kuona simpati nilimpigia Mbowe
(Freeman- Mwenyekiti wa Chadema Taifa), lakini simu yake iliita kama
vile mtu yupo nje ya nchi,” alifafanua Mwigulu.
Hata
hivyo, alisema amemuagiza IGP awaagize polisi kumtafuta Saanane na
kuhakikisha ufumbuzi wa kupotea kwake unapatikana na kujulikana alipo.
Juzi,
Mwenyekiti wa Umoja wa Kizazi cha Kuhoji Tanzania (UTG), Malisa
Godlisten akizungumza na waandishi wa habari, aliipa Chadema na taasisi
za umma zenye dhamana ya usalama wa raia saa 72 kuanzia jana kuhakikisha
Saanane anapatikana na kueleza umma chanzo cha vifo vya watu hao saba
ambao miili yao ilikutwa kando ya mto Ruvu, Bagamoyo.
0 comments:
Post a Comment