Rais
wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein ameiagiza Wizara ya Elimu na Mafunzo
ya Amali kuongeza kasi ya kubadili mitaala katika shule za sekondari na
kuingiza somo la ujasiriamali kwa lengo la kuwaandaa wanafunzi kwa
maisha ya kujiajiri.
Pia,
alisema Serikali itaimarisha vyuo vya amali ili somo la ujasiriamali
liweze kuchukua nafasi katika mitaala na kuhakikisha wanafunzi
wanapomaliza masomo watoke wakiwa na uelewa mzuri wa namna ya
kujiajiri.
Akizungumza
katika kongamano la siku mbili na maonyesho ya wajasiriamali
linalofanyika katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi, Kikwajuni mjini
Unguja, alisema utaratibu huo utawapa elimu itakayowasaidia kujiajiri
watakapokuwa wamemaliza masomo.
Dk
Shein aliwakumbusha vijana kuwa elimu waliyoipata katika vyuo vikuu na
taasisi mbalimbali zinazotoa mafunzo ya kazi na ufundi, wachukulie ni
mtaji muhimu katika kuendeleza shughuli za ujasiriamali.
Hivyo,
aliwataka wasijenge dhana kuwa ujasiriamali ni kufanya biashara
ndogondogo za bidhaa zinazoonekana katika masoko, lakini wajifunze
kutokana na uzoefu wa nchi mbalimbali hasa India ambapo vijana wengi
waliosoma wamekuwa wakijiajiri baada ya kumaliza masomo yao.
Alisisitiza
kuwa Serikali inatambua umuhimu wa kuwaendeleza wajasiriamali katika
kuyafikia malengo ya kupambana na umaskini wa kipato na kupunguza tatizo
la ajira, hasa miongoni mwa wanawake na vijana.
Dk
Shein alitumia fursa hiyo kueleza mafanikio ya Mfuko wa Uwezeshaji
ambao katika kipindi cha miaka miwili tangu ulipoanza umetoa jumla ya
mikopo 998 yenye jumla ya Sh1.6 bilioni, kwa visiwa vyote vya Unguja na
Pemba na hadi sasa marejesho ni asilimia 96.
Alisema
taarifa zinaonesha kwamba asilimia 67 ya watu waliopewa mikopo ni
vijana wenywe umri kati ya miaka 18 hadi 35, huku akiwataka wanasiasa
kutowadanganya vijana kuhusiana suala la ajira kwani vijana hivi sasa
hawadanganyiki.
Waziri
wa Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto, Maudline
Castico alisema kuwa kongamano hilo ni la kwanza la aina yake kufanyika
visiwani humo na kueleza kuwa mchango wa sekta binafsi kupitia
wajasiriamali wakubwa na wadogo ni muhimu ili kufikia lengo la Zanzibar
kuwa na uchumi wa kati ifikapo 2020.
Alisema
kuwa kongamano hilo linatarajiwa kuhamasisha na kuwaelimisha
wajasiriamali ili kuendeleza shughuli zao kwa ufanisi zaidi.
0 comments:
Post a Comment