Mzee Kingune Ngomale Mwiru
akizungumza na waandishi nyumabni kwake Victoria leo jijini Dar es
salaam kuhusu kukatwa kwa jina la Lowassa kwenye Uteuzi wa jina la
Mgombea wa Urais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CCM
…………………………………………………………………………
Utaratibu uliotumika kumteua
mgombea urais wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM),
umekosolewa na mwanasiasa wa siku nyingi Kingunge Ngombale Mwiru kwa
madai Kamati ya Maadili haikuwa na maadili kwa kumwengua Edward Lowassa.
Amesema hayo leo nyumbani
kwake jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari
akelezea alichokiita kuparaganyika kwa CCM kutokana na kukatwa jina la
mwanachama aliyemwamini ndiye anafaa kuongoza chama na serikali.
Katika kuonyesha ameudhika na
kamati zilizoundwa na chama hicho kupitisha na kukata wagombea, Kingunge
amesema anasikitika kuona Tanzania ni nchi yenye watu wapole wasiojua
kulalamika wala kuhoji hivyo amejitokeza kuhoji kwa niaba yao.
“Lakini yaliyotokea Dodoma
safari hii ni mapya, kazi ya kupeleka majina matano ilifanywa na chombo
kisicho na mamlaka, Kamati Kuu ilipewa majina bila kuwahoji wagombea.
Kamati ya Maadili ni kitengo tu hakina nguvu zaidi ya Kamati Kuu, NEC au
mkutano mkuu.
“Kitendo cha kuinyang’anya
Kamati Kuu mamlaka yake ni kibaya, wanajiita kamati ya maadili wakati
kamati yenyewe haina maadili, hii nchi ni yetu sote hata chama ni chetu
sote wachache tuliowapa madaraka ndani ya chama na serikali wanadhani
nchi ni yao,” alisema Kingunge.
Aliweka wazi kuwa anawaheshimu
viongozi wastaaafu Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Amani Abeid
Karume kutokana na umahiri wao waliouonyesha katika mchakato huo lakini
akadai nao wamepotoshwa kwa sababu wameshinikizwa kulikata jina la
Lowassa kutokana na taarifa zisizo sahihi.
Akikumbushia yaliyotokea katika
mchakato wa kutafuta mgombea wa CCM mwaka 1995, Kingunge alisema
“yalipoletwa majina sita katika mkutano wa NEC mwaka 1995 yalionekana
majina ya Benjamin Mkapa, Jakaya Kikwete, Pius Msekwa, Cleopa Msuya,
Mark Bomani na Joseph Warioba. Wajumbe wakahoji jina la Lowassa liko
wapo.
“Lowassa alijiuzulu kuwajibika
kisiasa lakini pia likageuzwa na watu kuanza kuimba wimbo wa ufisadi,
mimi nilipoona anaonewa nikaamua kukaa kimya na kumshauri ajiuzulu kwa
sababu nilishapata taarifa kuwa wanataka kumchafua. Nikamwambia kabla
lengo lao halijatimia bora ajiuzulu kulinda hadhi na mustakabali wake
kisiasa.”
Aliongeza kuwa Lowassa
anakubalika ndani nje ya chama, hata kashfa anazopewa kuwa alitumia
fedha nyingi wakati wa kutangaza nia hadi kurudisha fomu si za kweli
anasingiziwa tu, Kingunge anamtaja kada huyo amelelewa na chama hivyo
anakijua vema kuliko wagombea wengine waliopita kwenye tano bora.
“Tunapomtafuta rais kupitia CCM
ikumbukwe pia tunamtafuta mwenyekiti wa chama, maana yake tukimpata
mgombea mwingine inabidi tuwe na kazi ya ziada kujifunza masuala ya
chama. Mkasa huu wa viongozi wa chama na serikali kutumia nguvu nyingi
kuzuia mapenzi ya wananchi wajue kuwa huyo waliyemkusudia hawatampata,”
alisema.
Alipoulizwa ikiwa anakubali
uteuzi wa Joseph Magufuli, alisema kwa sasa hana budi kuwaomba wanachama
wote kuunga mkono uteuzi huo kwani walioingia katika tano bora hawana
makosa hata wao walichaguliwa tu.
Kingunge ametoa angalizo kuwa
baada ya uchaguzi kuisha lazima suala hilo lijadiliwe kwa sababu chama
kimegawanyika vipande vipande kutokana na mgombea aliyekubalika na
wanachama wengi kukatwa bila kufuata taratibu.
“Kwa upande wangu naona ni kama
Lowassa ndiye aliyeshinda katika ushindani huu kwa sababu watu ndaNi na
nje ya nchi wameona namna anavyokubalika, Lowassa ni kipenzi cha watu
na hakuna kitu kizuri kama kupendwa,” alisema.
0 comments:
Post a Comment