Tume ya
Uchaguzi nchini Gambia imemtangaza mgombea wa upinzani, Adama Barrow,
kuwa mshindi wa uchaguzi wa rais uliofanyika Jumapili na kuna taarifa
kuwa tayari Rais Yahya Jameh amekubali kushindwa.
"Ni jambo
la kipekee kwamba mtu ambaye ametawala nchi hii kwa kipingi kirefu kama
hiki amekubali kushindwa," mwenyekiti wa tume ya uchaguzi, Alieu Momar,
aliwaambia waandishi wa habari muda mchache kabla ya kutaja rasmi
matokeo ya uchaguzi huo mjini Banjul hivi leo (Ijumaa, Novemba 2).
Tume hiyo ya uchaguzi inasema Barrow amepata asilima 45.5 ya kura, huku Jammeh akipata asilimia 36.7.
Jammeh,
ambaye mara moja alikuwa amesema kuwa angelitawala kwa miaka bilioni
moja Mungu akipenda, alikuwa akijaribu kuwania wadhifa huo kwa mara ya
tano kupitia chama chake cha Alliance for Patriotic Reorientation and
Construction (APRC).
Televisheni
ya taifa ya Gambia ililiambia shirika la habari la AFP kwamba Jammeh
angelitoa taarifa yake baadaye kumpongeza Barrow.
Barrow,
mwenye umri wa miaka 51, alikuwa ni mfanyabiashara asiyejuilikana sana
lakini akateuliwa na muungano wa upinzani kupambana na Jammeh aliyekaa
madarakani kwa miaka 22, akijikuta kuwa ana ufuasi mkubwa uliokuwa
haukutazamiwa.
Barrow kuongoza serikali ya mpito
Ikiwa
kweli Rais Jammeh atatangaza kushindwa, Barrow anatazamiwa kuhudumu
muhula wa miaka mitano akiongoza serikali ya mpito kuelekea mageuzi
rasmi ya kidemokrasia kwenye koloni hilo dogo la zamani la Uingereza,
maarufu kwa fukwe zake.
Meneja wa
kampeni wa Jammeh, Yankuba Colley, alisema hakuwa akijuwa chochote
kuhusiana na tangazo la mwenyekiti wa tume ya uchaguzi, lakini alikuwa
na hakika kuwa kama raia wa Gambia wameamua rais huyo aondoke, basi
ataondoka.
"Ikiwa
watu wa Gambia wametoa hukumu yao, yeye ni muumini mzuri," aliliambia
shirika la habari la AFP, akiongeza kuwa: "Ni matokeo mabaya lakini mtu
ninayemjuwa mimi atakubali vyovyote yatakavyokuwa."
Timu ya Barrow ilithibitisha tangazo la Tume ya Uchaguzi.
Uchaguzi
huo wa Alhamis ulikumbwa na kuzimwa kwa huduma za Intaneti, hatua
iliyosababisha lawama kali kutoka makundi ya haki za binaadamu na
Marekani.
Lakini
matokeo ya awali asubuhi ya Ijumaa yalikuwa mazuri kwa Barrow, baada ya
kuutwaa mji mkuu, Banjul, ambao awali ulikuwa ngome madhubuti kwa
Jammeh.
Barrow
alishinda takribani asilimia 50 ya kura kwenye majimbo matatu ya Banjul
kwa mujibu wa tume ya uchaguzi, ikilinganishwa na asilimia 43 za Jammeh.
Vikosi vya usalama vilimiminwa kwa wingi mitaani, kukiwa na wasiwasi kwamba huenda Jammeh asingekubali matokeo ya kura hiyo.
Hadi
nyakati za alfajiri, wanajeshi, polisi na maafisa wa vyombo vyengine vya
usalama walionekana kwenye vizuizi vya barabarani, huku raia wakisalia
majumbani mwao kufuatilia matokeo.
0 comments:
Post a Comment