Monday, 7 November 2016

CCM Yatuma Salamu Za Rambi Rambi Kifo Cha Mzee Samwel Sitta

...

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimepokea kwa majonzi na simanzi kubwa taarifa za kifo cha Mhe. Samuel John Sitta, Spika mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kilichotokea usiku wa jana tarehe 6/11/2016 katika hospitali ya Technical University of Munich nchini Ujerumani alipokuwa akitibiwa.

Mhe. Samuel John Sitta, amewahi kushika nyadhifa mbalimbali za utumishi katika Chama na Serikali. Alikuwa Katibu wa CCM na Mkuu wa Mkoa, Mkurugenzi Mkuu wa kituo cha uwekezaji, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Mjumbe wa Kamati Kuu, Mbunge, Waziri na Spika.

Mhe. Sitta alikuwa ni Kiongozi mchapakazi, mwadilifu na aliyejitambulisha kwa utendaji wenye kufuata falsafa yake ya “kasi na viwango”. Ametoa mchango mkubwa katika ujenzi wa Chama na Serikali.

Katibu Mkuu wa CCM Ndg Abdulrahman Kinana amemtumia salamu za rambi rambi Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai, familia ya Mhe. Sitta pamoja na Wananchi wa Jimbo la Urambo kufuatia kifo cha Kiongozi huyu. Tunaungana nao katika msiba huu ambao pia ni msiba wetu

Mwenyezi Mungu aiweke roho ya marehemu mahali pema peponi, Ameni

Imetolewa na:-
CHRISTOPHER OLE SENDEKA (MNEC)
MSEMAJI WA CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM)

07 – 11 – 2016
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger