Wakili wa Serikali, Patrick Mwita amemuomba radhi Hakimu Mkazi Mkuu wa
Kisutu kwa kushindwa kutekeleza amri ya kumkamata mbunge wa Singida
Mashariki (Chadema), Tundu Lissu anayekabiliwa na kesi ya uchochezi
pamoja na wahariri wa gazeti la Mawio.
Wakili Mwita alifanya
hivyo jana baada ya hakimu huyo, Thomas Simba kumuhoji sababu za
kushindwa kutekeleza amri hiyo wakati hati ya kumkamata ilitolewa
Novemba 3, 2016 na wakili huyo kuisaini. “Kwa nini hamkumkamata” Si
mlikuwa na wajibu wa kumkamata? Mnamuogopa?” alihoji hakimu huyo.
Hata
hivyo, pamoja na kuomba radhi hiyo mahakama imechukua hati ya kusafiria
ya Lissu ili kudhibiti safari zake nje ya nchi kwa kuwa amekuwa
akisafiri bila kuitaarifu mahakama.
Katika kesi hiyo, Lissu na
watu wengine watatu wameshtakiwa kwa makosa matano ya uchocheza kutokana
na habari iliyochapishwa na gazeti la Mawio kuhusu hali ya kisiasa
Zanzibar.
Hakimu Simba ameahirisha kesi hiyo hadi Novemba 28, 2016 na washtakiwa wote wapo nje kwa dhamana.
Kabla ya uamuzi huo, Wakili Mwita alisema jana ilikuwa siku ya kesi hiyo kutajwa na kwamba upelelezi unakaribia kukamilika.
Kuhusu
madai ya kudharau mahakama Wakili Peter Kibatala anayemwakilisha Lissu
aliiambia mahakama kuwa mteja wake yupo mahakamani, hivyo ametii amri ya
mahakama na kwamba jukumu la dhamana ni kuhakikisha mshtakiwa anakuwapo
mahakamani wakati wa kesi yake na kwamba uwepo wake ni kutii masharti
ya dhamana.
Hata hivyo, Wakili Mwita alidai kuwa kitendo cha
Lissu kutofika mahakamani mara mbili mfululizo ni kama kuonyesha dharau
kwa mahakama hiyo.
Mwita alidai kuwa Lissu ni mwanataaluma wa
sheria na anafahamu taratibu za kufuatwa kama hafiki mahakamani na
kwamba mdhamini si mbadala wa mshtakiwa mahakamani.
“Alipaswa
kuandika barua kuitaarifu mahakama hii kama wakili kuwa ana kesi ya
uchaguzi anayoiendesha Bunda na kuambatanisha na samansi ama orodha ya
kesi. Tunaomba mahakama iheshimiwe na jukumu la kumfutia dhamana ama
kutokumfutia dhamana Lissu bado lipo mikononi mwako mheshimiwa,”
alieleza wakili huyo wa Serikali.
Akizungumzia hoja hizo, Hakimu
Simba alisema Lissu ni wakili maarufu, msomi na anajua taratibu zote za
mahakama, lakini wadhamini wake wanababaika, hivyo alimtaka aeleze
sababu za kwenda Ujerumani bila kutoa taarifa mahakamani.
Lissu
alijibu kuwa hakuwa na nia ya kuidharau mahakama, wala kuikimbia kesi
inayomkabili bali alikwenda Ujerumani katika mazingira ya dharura.
Hakimu
Simba alimwambia mahakama inafahamu kesi za uchaguzi na maelekezo yake,
hivyo ikamuuliza sababu za kutotoa taarifa wakati alipokwenda
kushughulikia kesi ya Bunda
“Nilipopata taarifa ya kwenda kuiendesha
kesi hiyo ilikuwa ni siku moja baada ya kutoka nchini Ujerumani na
kwamba niliandika barua ya kuitaarifu mahakama na nilituma iletwe
mahakamani kupitia wasaidizi wangu,”alisema Lissu.
Lakini
Hakimu Simba alisema: “Hakuna barua iliyotufikia. Usituingize katika
migogoro kutokana na nafasi yako katika jamii ya mwanasheria.
Hatukuogopi labda upande wa mashtaka ndio wamekuogopa.
“Tunataka
kufuata mfumo, hatutakuogopa na wala hatutakuonea. Hapa naona upande wa
mashtaka wanapiga blaa blaa, tuelewane tunaichukua hati yako ya
kusafiria ili ukitaka kusafiri tujue.”
0 comments:
Post a Comment