WANAFUNZI 526,653 sawa na asilimia 94.8 ya waliofaulu mtihani wa darasa
la saba mwaka huu, wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwakani
katika shule za sekondari za serikali katika awamu ya kwanza huku 28,638
wakishindwa kupangiwa shule katika awamu ya kwanza.
Kati ya wanafunzi hao, wasichana ni 268,052 sawa na asilimia 94.5 ya
wasichana waliofaulu na wavulana ni 258,601 sawa na asilimia 95.2 ya
wavulana waliofaulu. Wanafunzi waliosajiliwa kufanya mtihani wa darasa
la saba mwaka 2016 walikuwa 795,739, huku 244 wakifutiwa matokeo ya
mtihani kutokana na udanganyifu.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari jana mjini hapa, Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais anayeshughulikia Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene alisema wanafunzi waliochaguliwa
wamegawanyika katika makundi manne likiwemo la shule za bweni kwa wenye
ufaulu mzuri ambao waliochaguliwa ni 900 wavulana 480 na wasichana 420.
Alisema kwa shule za bweni za ufundi waliochaguliwa ni 1,005, shule za
bweni kawaida ni 780, shule za bweni kwa wenye ulemavu ni 723 na shule
za kutwa wanafunzi waliochaguliwa ni 523,245. Alisema jumla ya wanafunzi
3,408 sawa na asilimia 0.6 wamechaguliwa kwenda sekondari za bweni.
Jumla ya watahiniwa 555,291 walifaulu sawa na asilimia 70.36 ya
wanafunzi waliofanya mtihani, kati yao wasichana ni 238,753 sawa na
asilimia 51.1 na wavulana 271,538 sawa na asilimia 48.9.
Ufaulu umeongezeka kwa asilimia 2.52 ukilinganisha na asilimia 67.84 kwa
mwaka 2015. Simbachawene alisema katika uchaguzi huo, wanafunzi 28,638
hawakuchaguliwa katika awamu ya kwanza, na kuitaja mikoa ambayo
wanafunzi wamebaki ni Dar es Salaam (18,820), Arusha (4,752), Songwe
(1,465), Kigoma (1,208), Manyara (1,141), Lindi (608), Mbeya (406) na
Katavi (238).
Aidha, waziri huyo alisema kati ya wanafunzi 1,060,588 walioanza darasa
la kwanza 2010, wanafunzi waliosajiliwa kufanya mtihani wa darasa la
saba mwaka 2016 ni 795,739 sawa na asilimia 75 ya wanafunzi
walioandikishwa wakiwemo wasichana 422,562 sawa na asilimia 53.1 na
wavulana 373,177 sawa na asilimia 46.9 ya waliosajiliwa.
Akizungumzia udanganyifu, alisema watawavua madaraka kwa waliokuwa
waratibu elimu kata na walimu wakuu, kuwashitaki mahakamani na kupeleka
mashauri yao Tume ya Utumishi ya Walimu, baada ya udanganyifu kuongezeka
ambako watahiniwa 244 wamefutiwa matokeo mwaka 2016 ikilinganishwa na
wanane wa mwaka jana.
Alizitaja shule zilizohusika kwenye udanganyifu huo ni Shule ya Tumaini
na Little Flower za Sengerema mkoani Mwanza, Mikahamakumi iliyopo
Sikonge, Tabora ambazo ni za binafsi, wakati za serikali ni Kondi
Kasandalala iliyopo Sikonge, Tabora, Qash iliyopo Babati na St Getrude
iliyopo Madaba mkoani Ruvuma.
Aidha, alisema 10 bora za serikali ni Kazunzu iliyopo Halmashauri ya
Buchosa (Mwanza), Mwanahegele ya Maswa (Simiyu), Huruma ya Mbinga
(Ruvuma), Kabanga ya Ngara (Kagera), Butumba B (Jiji Mwanza), Masoko ya
Kilwa (Lindi), Lyambamgongo ya Bukombe (Geita), Kilimani ya Geita
Vijijini, Magufuli ya Chato na Nkome ya Geita Vijijini, Geita.
Alisema shule 10 zilizofanya vibaya ni Chohelo ya Mvomero (Morogoro),
ambayo ni ya mwisho kitaifa ikifuatiwa na shule za Iloliento, Longido
(Arusha), Mwalebi na Nchilila Meatu (Simiyu), Magingi ya Mvomero, Kilole
ya Lushoto, Tanga, Zege ya Korogwe, Tanga na shule tatu za Lubchi,
Kitengo na Mgata za Morogoro vijijini.
0 comments:
Post a Comment