Hatimaye
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam imemwachia huru
Mbunge wa Sumve (CCM), Richard Ndassa (56) baada ya upande wa Jamhuri
kuomba kumuondolea kesi kushawishi na kuomba rushwa ya Sh.milioni 30.
Ndassa
alikuwa anakabiliwa na shtaka la kushawishi na kuomba rushwa kutoka
kwa Mkurugenzi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Felichesmi
Mramba.
Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dennis Lekayo jana aliwasilisha maombi ya kumwondolea Ndassa mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Victoria Nongwa.
Lekayo
alidai kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP), ameona hana nia ya
kuendelea na mashtaka yaliyopo mahakamani dhidi ya mshtakiwa chini ya
kifungu cha 98 (a) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA).
Aidha
kwa mujibu wa kifungu hicho kinampa mamlaka DPP ya kumwondolea mashtaka
mtuhumiwa kabla ya kusikiliza ushahidi lakini anaweza kukamatwa na
kushtakiwa upya.
Hakimu
Nongwa alisema kwa kuwa upande wa Jamhuri umeomba kumwondolea mshtakiwa
mashtaka na kwamba hawana nia ya kuendelea na kesi hiyo, mahakama yake
imekubali ombi hilo.
"Mahakama
hii inamwachia mshtakiwa chini ya kifungu cha 98 (a) kama upande wa
Jamhuri ulivyowasilisha maombi yao dhidi ya mshtakiwa" alisema Hakimu
Nongwa.
Mapema
mwaka huu, Mbunge huyo ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya kudumu ya
Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma, alifikishwa mahakamani hapo na
kusomewa shtaka la kushawishi na kuomba rushwa ya Sh. milioni 30.
Katika
kesi ya msingi, Lekayo alidai kuwa Machi 13, mwaka huu, jijini Dar es
Salaam, Ndassa aliomba rushwa Sh.milioni 30 kutoka kwa Mramba.
Ilidaiwa
kuwa aliomba rushwa ili awashawishi wajumbe wenzake wa kamati hiyo
watowe mapendekezo mazuri katika mahesabu ya fedha ya Tanesco kwa mwaka
wa fedha 2015/2016.
Katika
shitaka la pili, mwakilishi huyo wa wananchi siku ya tukio la kwanza
pia aliomba rushwa ya huduma ya umeme kwa kumshawishi Mramba atowe
huduma hiyo kwa ndugu wa mbunge huyo Matanga Mbushi,Richard Ndassa na
rafiki wa ndugu yake Lameck Mahewa.
Mbunge huyo alikana mashitaka yake na alikuwa nje kwa dhamana.
0 comments:
Post a Comment