Monday, 14 November 2016

Vyoo 100 kujengwa barabara ya Mwanza Kwenda Dar Es Salaam

...

Taasisi  ya The Desk & Chair Foundation (TD& CF), inatarajia kujenga vyoo 100 katika Barabara Kuu ya Mwanza-Shinyanga-Dar es Salaam unaokadiriwa kutumia Sh. milioni 500.

Mwenyekiti wa TD & CF, Alhaji Sibtain Meghjee alisema hivi karibuni mjini Mwanza kwamba mradi huo ni sehemu ya miradi mitatu mikubwa ambayo taasisi yake inatekeleza nchini.

Alisema baada ya kukamilisha mradi mkubwa wa  jengo la kupumzikia wananchi wanaokwenda kutibiwa na kuwajulia hali wagonjwa waliolazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza, Sekou Toure wanatarajia kujenga vyoo 100 kwenye barabara ya kutoka Mwanza hadi  Dar es Salaam kwa basi.

Meghjee alieleza kuwa maandalizi ya awali ya mradi huo yameshaanza na kwamba watashirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (SUMATRA) na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) ili kupata taarifa sahihi kabla ya mradi kuanza.

“Penye nia pana njia, baada ya kukamilisha ndoto yetu, leo ya mradi huu mkubwa wa ujenzi wa jengo la kupumzikia hapa Sekou Toure, tunatarajiwa kutekeleza miradi mitatu mikubwa ukiwemo wa vyoo  kwa ajili ya abiria wanaosafiri kati ya Mwanza na Dar es Salaam:

“Tunataka msamiati wa kuchimba dawa wakati wa safari ubaki kuwa historia kwa hiyo tunatarajia kufanya jaribio moja la kujenga matundu 100 ya vyoo katika njia na barabara kuu ya Mwanza hadi Dar es salaam ambavyo vitagharimu shilingi milioni 500.Tutashirikiana na mamlaka husika, ofisi yako na idara ya afya,”alisema Meghjee.

Meghjee alieleza kuwa taasisi hiyo pia ina mpango wa kutekeleza mradi wa kutengeneza viungo bandia kwa kushirikiana na kitengo cha Jairpur Foot/Knee and Limb Project cha India ambao unahitaji Dola 200,000 za Marekani (sh. milioni 44), zitakazowezesha kuanzisha huduma ya viungo hivyo bandia vya miguu, mikono, fimbo na baiskeli.

Alisema wanaendelea kuwasiliana na wafadhili watakaoshirikiana nao kwenye mradi huo na kuwahakikishia walengwa kuwa viungo hivyo vitapatikana kwa gharama nafuu mara utakapokamilika mradi huo.

Meghjee aliongeza kuwa wakati wakiendesha ujenzi wa jengo la mapumziko katika Hospitali ya Sekou Toure,walipata wazo la kujenga mabanda yatakayotumiwa na madereva wa pikipiki (boda boda) kuegesha vyombo vyao kivulini na kupata huduma ya vyoo na mabafu.

Mwenyekiti huyo wa TD & CF aliongeza zaidi kuwa endapo Halmashauri ya Jiji itaridhia na kuwapa eneo maalumu na mahususi la ujenzi wa huduma hiyo watafanya jaribio hilo moja ili kuweza kuona matunda yake.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger