Monday, 28 November 2016

RAIS Magufuli Ampongeza Paul Makonda

...

RAIS John Magufuli amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kwa juhudi za kusikiliza na kutatua kero za wananchi.

Magufuli ametoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na Mkuu huyo wa Mkoa huo kwa njia ya simu wakati Makonda akiendelea na mkutano wa hadhara katika eneo la Mbezi Maramba Mawili jijini humo.

Amesema, juhudi anazozifanya Makonda ni za kuigwa na viongozi wengine katika mikoa yao kwani anasaidia kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi.

“Wananchi wana kero nyingi sana, lakini viongozi wao wangekuwa wanawasikiliza hata maswali wanayouliza hapo yasingeulizwa, nakupongeza sana Mkuu wa Mkoa natamani na viongozi wengine wangeiga mfano wako,”amesema Magufuli.

Rais alipigiwa simu na Makonda ili asaidie kutoa ufafanuzi kuhusu upana wa barabara zilizopo chini ya Wakala wa Taifa wa Barabara (Tanroads) baada ya wananchi kulalamikia kuvunjiwa maeneo yao ili kupisha ujenzi.

Katika ufafanuzi wake, Rais Magufuli alisema suala la barabara kutoka Ubungo hadi Ruvu tayari wameshalitolea ufafanuzi mara nyingi.

Amesema akiwa Waziri wa Ujenzi wakati serikali inataka kupanua barabara ya kutoka Ubungo kwenda Kibaha kulitokea malalamiko ya aina hiyo na kesi kuhusu suala hilo namba 137 ilifikishwa mahakamani ambapo serikali ilishinda na baadaye yalitolewa maelekezo kuhusu maeneo yaliyopo katika hifadhi ya barabara.

Amesema baada ya ushindi huo kutoka Mahakama Kuu walichukua hatua ya kubomoa nyumba zote zilizokuwa katika hifadhi ya barabara kwa mujibu wa sheria ya mwaka 1932 ambayo ilifanyiwa marekebisho mwaka 1949 ikafanyiwa tena marekebisho mwaka 1954 na mwaka 1965.

Amesema Sheria ya Ardhi namba 4 ya mwaka 1999 na Sheria ya Vijiji namba tano ya mwaka 1999 na Sheria ya Mipango Miji na Matumizi ya Ardhi ya mwaka 2007 zote zinatambua hifadhi ya barabara na kwa barabara ya Dar es Salaam kwenda Kibaha iliachwa kwa upana uliopo kama filta ya Jiji la Dar es Salaam.

“Mwito wangu kwa wananchi wazingatie sheria na sheria ni msumeno, tulitunga sheria sisi wenyewe hivyo ni wajibu wetu sisi serikali kusimamia sheria, lakini kama wanaona sheria haifai ni kiasi cha kwenda kulishauri Bunge libadilishe sheria ili barabara ya Ubungo iwe sentimita tano zipite bajaji tu, lakini ukweli unabaki palepale kwamba sheria ipo na haijawahi kubadilishwa,”amesema Rais Magufuli.

Aidha Magufuli aliipongeza Tanroads kwa kusimamia sheria kwani alisema itafika kipindi kutakuwa hakuna barabara nchini.

Rais Magufuli amesema pia kazi ya kuvunja nyumba zilizopo katika hifadhi ya barabara ipo pale pale kwa vile serikali imepata kiasi cha Sh bilioni 67 za kujenga barabara zinazobadilishana (interchange) katika eneo la Ubungo ambayo itakuwa ya ghorofa mbili au tatu ili kurahisisha usafiri.

“Ghorofa zote na majengo yatavunjwa bila fidia hata kama litakuwa jengo la Tanesco kwa sababu lazima tuzingatie sheria, lakini kama wananchi wataona wameonewa basi waende mahakamani,” alisema.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger