WAHITIMU, viongozi na wageni waliohudhuria Mahafali ya 32 ya Chuo Kikuu
cha Sokoine cha Kilimo (SUA) mkoani Morogoro, waliingiwa na simanzi
wakati mtoto, Tamar Aaron Mbogho (11), alipojitokeza na kupokea Shahada
ya Udaktari wa Falsafa (PhD), akimwakilisha mama yake Swai Sophia
Faustin ambaye alifariki dunia miezi sita kabla ya kufika siku ya
mahafali.
Tamar, mtoto pekee wa marehemu, ambaye baba yake mzazi ni Mkuu wa Wilaya
ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro, Aaron Mbogho alifika katika hafla hiyo
akiwa ameambatana na ndugu zake kadhaa, tayari kwa ajili ya kupokea
heshima hiyo kwa niaba ya mama yake.
Gazeti hili liliweza kuwasiliana kwa njia ya simu na Mbogho akiwa katika
kituo chake cha kazi Mwanga ambapo alisema Tamar alifika katika hafla
hiyo kupokea shahada hiyo kwa niaba ya mama yake.
Kwa mujibu wa Mbogho, mkewe Dk Sophia alifariki dunia Mei 21, 2016,
wakati huo akiwa ameshahitimu masomo yake kikamilifu na alisema Tamar ni
mtoto wa pekee wa Sophia.
"Alikuwa ni mmoja wa wahitimu waliopaswa kutunukiwa shahada hiyo kwa
sababu tayari alishahitimu na kubakia muda wa mahafali, lakini bahati
mbaya akafariki dunia kabla ya muda kuwadia,” alisema na kuongeza.
"Binti yetu alipenda kwenda kuchukua shahada ya mama yake na
alisindikizwa na ndugu zake wa familia. Ameniambia malengo yake ni
kusoma kwa bidii ili aweze kupata Shahada ya Udaktari wa Falsafa kama
mama yake, " alisema Mbogho.
Katika mahafali hayo yaliyofanyika juzi katika Kampasi ya Solomon
Mahlangu, Mazimbu, wahitimu 61 walifuzu na kutunukiwa Shahada ya
Udaktari wa Falsafa ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo.
Naibu Makamu Mkuu Taaluma wa Chuo Kikuu hicho, Profesa Peter Gilla,
alisoma orodha ya watunukiwa ambapo pia alitaja jina la mwanafunzi
asiyekuwapo ambaye alifariki dunia, lakini akiwa amefuzu na anastahili
kupata Shahada ya PhD ya Chuo Kikuu hicho ambaye ni Sophia.
Hivyo, Mwenyekiti wa Mahafali hayo, Dk Benno Mrembuka, alimwongoza mtoto
Tamar kwenda kupokea shahada hiyo kutoka kwa Naibu Makamu Mkuu wa Chuo
Fedha na Utawala, Profesa Yonika Ngaga, hali iliyoleta simanzi na huzuni
kwa washiriki waliokuwepo katika mahafali hiyo.
Baadaye Tamar alielekezwa kufika mbele ya meza kuu ili kuwapa mkono
wageni mbalimbali ambao walitumia nafasi hiyo kumfariji kutokana na
kumpoteza mama yake mzazi ambaye alikuwa ni mhitimu.
Katika hatua nyingine, Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu hicho, Profesa
Gerald Monela, alisema SUA imeendelea kutoa wahitimu wa Shahada ya
Sayansi na Ualimu katika masomo ya sayansi kwa ajili ya kukidhi mahitaji
makubwa ya walimu wa kufundisha shule za sekondari nchini.
0 comments:
Post a Comment