Wednesday, 30 November 2016

FAHAMU JINSI FEDHA ZA TETEMEKO LA ARDHI MKOANI KAGERA ZILIVYOTUMIKA

...



Ndugu zangu kama ambavyo tunakumbuka Tarehe 10/09/2016 majira ya saa 9 na dakika 27 Alasiri maeneo ya Kanda ya ziwa hasa Mkoani Kagera kulitokea tetemeko la ardhi linalokadiriwa kuwa na ukubwa wa 5.9 katika vipimo vya Richter ambapo Kitovu cha tetemeko hilo ni kwenye makutano ya latitudo 10 06’ na longitudo 31055’ eneo ambalo ni kilomita 20 kaskazini mashariki mwa kijiji cha Nsunga na kilomita 42 kaskazini magharibi mwa mji wa Bukoba na Kitovu hicho kilikuwa kilomita 10 chini ya ardhi kwenye eneo hilo.

Tetemeko hilo la ardhi liliacha familia kadhaa zikiwa na huzuni kubwa kwa kuwapoteza ndugu, jamaa na rafiki zao ambapo idadi ya watu waliofariki walikuwa ni 17 huku watu 560 wakipatiwa matibabu kutokana na majeraha waliyoyapata sambamba na kukutikana kwa uharibifu wa makazi na miundombinu ya umma na watu binafsi.

Kwa Mujibu wa Mtendaji Mkuu, Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) alieleza sababu za kutokea kwa Tetemeko hilo la ardhi kuwa ilikuwa ni kutokana na kitovu cha tetemeko hilo kuwa kiko chini sana ya ardhi (Km 10) na kwa kutafasiri umbile la mawimbi ya tetemeko hilo yaliyonakiliwa na vituo vya kupimia matetemeko ya ardhi inaonekana kuwa tetemeko hilo limetokana na misuguano ya mapange makubwa ya ardhi iliyopasuliwa na mipasuko ya ardhi mithili ya mipasuko kwenye bonde la ufa. 

Kwa kuwa eneo lililokumbwa na tetemeko la ardhi liko karibu na mkondo wa magharibi wa bonde la ufa la Afrika Mashariki inakisiwa kuwa mtetemo huo ulisababishwa na kuteleza na kusiguana kwa mapande ya miamba juu ya mipasuko ya ardhi ya bonde hilo la ufa.

Katika siku za karibuni kumekuwepo na taarifa mbalimbali katika mitandao ya kijamii ikiwemo facebook, Twitter, Blogs, Instagram na Makundi mbalimbali ya Watsup jambo ambalo lilinilazimu kufunga safari na kuweka kambi ya takribani siku nne Mkoani Kagera ili kubaini ukweli wa namna fedha zilizopatikana na zilivyotumika ikiwa ni pamoja na mahitaji mengine jinsi yalivyopatikana na namna yalivyoelekezwa.

UKWELI WA MAMBO

Kufuatia tathmini zilizofanyika kupitia wataalamu mbalimbali, makadirio ya awali yalibaini kuwa kiasi cha jumla ya shilingi Bilioni 104.9 zinahitajika katika kukabiliana na kurejesha hali katika Mkoa wa Kagera kufuatia maafa hayo. Ambapo gharama hizi zinajumuisha:

a) Ujenzi wa makazi ya muda kwa waathirika wa nyumba zipatazo 16,667 zilizoharibika katika viwango tofauti, ambapo kiasi cha Shilingi Bilioni 41.7 zitahitajika.

b) Kiasi cha shilingi 1.92 kwa ajili ya kodi ya miezi sita kwa wapangaji waliokuwa wakiishi kwenye nyumba zilizoharibiwa.

c) Ukarabati wa shule za msingi 163 kwa gharama ya shilingi Bilioni 12.7, sekondari 57 kwa gharama ya shilingi Bilioni 45.65, vituo vya afya na zahanati 32 kwa gharama ya shilingi milioni 772 na Majengo ya taasisi nyingine 20 kwa shilingi Bilioni 1.3

MISAADA ILIYOTOLEWA

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Katibu Mkuu (WAZIRI MKUU NA BUNGE) Ndg Uledi A. Mussa ilibainisha kuwa hadi kufikia Tarehe 13 Novemba, 2016 serikali ilikuwa imepokea misaada ya vifaa, Chakula, Fedha na ahadi mbalimbali zenye thamani ya shilingi Bilioni 15.19 kutoka kwa wadau mbalimbali, washirika wa Maendeleo, Balozi wan chi marafiki ambapo tayari misaada hiyo imeshagawiwa na inaendelea kusambazwa kwa walengwa. 

Msaada ya misaada iliyopokelewa ni kama ifuatavyo:

 Fedha taslimu kiasi cha shilingi Bilioni 5,412,934.82 kimeshapelekwa Benki.

 Kiasi cha shilingi milioni 17,579,427.00 kupitia mitandao ya simu

 Ahadi za shilingi Bilioni 6,703,000,000 Hivyo jumla ya ahadi na fedha taslimu hadi sasa ni Shilingi Bilioni 12,133,564,361.82

 Serikali pia imepokea misaada mingine yenye thamani ya shilingi Bilioni 2.25 kama ifuatavyo: Unga Tani 58.12, Sukari Mifuko 1,150, Mchele Tani 133.96, Maharagwe Tani 19.666. Mahindi Tani 70.1, Majani ya Chai Tani 3, Maji Katoni 1,570, Mafuta lita 6,022, Sabuni Katoni 443, Shuka 495, Blanketi 6,125, Vyandarua 2,821, Magodoro 1,146, Mahema 367 n Turubai 6,237 vilipokelewa. 

Aidha serikali ilipokea vifaa vya ujenzi vikiwemo Saruji mifuko 24,433, Bati 20,933, Misumari kilo 1475, Nondo vipande 725, Kofia za bati 150 na mbao 250.

Lakini ifahamike kuwa baadhi ya waaliotoa ahadi kama serikali ya Uingereza wameahidi kutekeleza ahadi zao kwa kujikita moja kwa moja katika ujenzi wa Shule, Mara baada ya wakala wa majengo kuainisha viwango na gharama.

HATUA ILIYOCHUKULIWA NA SERIKALI KATIKA KUKABILIANA NA MAAFA 

Katika siku za hivi karibuni kumekuwepo na juhudi za kujaribu kufanya upotoshaji kuhusu hatua zilizochukuliwa na zinazoendelea kuchukuliwa katika kukabiliana na maafa haya, Ukweli ni kwamba serikali kwa kushirikiana na wadau imechukua hatua kubwa za kuwasaidia waathirika ambapo miongoni mwao yafuatayo yameshafanyika:

 Kutoa matibabu bure kwa majeruhi wote 560, kuandaa na kugharamia mazishi ya watu 17 waliofariki ambapo Mheshimiwa Waziri Mkuu alihudhuria, Aidha serikali kwa kushirikiana na wadau ilitoa mkono wa pole wa Shilingi Milioni 1.8 kwa kila familia iliyopatwa na msiba.

 Kuendelea kutoa misaada mbalimbali ya kibindamu ikiwemo chakula, Madawa, Nguo, Makazi ya muda, Huduma za tiba, Vifaa vya shule na huduma ya ushauri wa kisaikolojia kwa waathirika katika Wilaya zote za Mkoa wa Kagera zilizopata athari.

 Kushirikiana na Ofisi ya Mwakilishi Mkazi mmoja wa Mataifa na wadau mbalimbali wakiwemo Msalaba Mwekundu, Plan International (T), BRAC (T), World Vision, CARITAS, Save the Childre, JH Piego na Benki ya Dunia kufanya tathmini ya pamoja ya mahitaji ya haraka ya athari za Tetemeko la ardhi ili kubaini maeneo zaidi ya kuwasaidia wananchi.

HATUA ZA KUREJESHA HALI

Tangu kutokea kwa maafa haya serikali imeendelea kufanyia kazi masuala muhimu yaliyoainishwa katika tathmini ya Tetemeko ambapo hadi kufikia tarehe 13 Novemba, 2016 licha ya kuendelea kuwapatia wananchi mahitaji muhimu kama Chakula, Dawa na Misaada ya kujikimu katika makazi ya muda, kiasi cha shilingi Milioni 969,238,326.35, Mifuko ya saruji 17,423, Bati 5,348 na Misumari Kilo 1,107 vilitumika kwa kufanya ukarabati mkubwa na mdogo wa shule za msingi na Sekondari, Juhudi ambazo ziliwezesha wanafunzi wa shule hizo waliokuwa katika hatari ya kukosa masomo kuendelea na masomo yao.

Gharama hizo pia zimejumuisha ukarabati wa zahanati katika Halmashauri za Mkoa wa Kagera na kuanza kwa ujenzi wa kituo kipya cha afya (Ishozi/Kabyaile) kitakachojumuisha chumba cha upasuaji wa wodi ya kina mama na watoto kwa faida ya wananchi wote wa maeneo hayo. Pia serikali imegharamia urejeshwaji wa miundombinu ya barabara, maji na umeme katika maeneo kadhaa yaliyoathiriwa na tetemeko.

Shirika la World Vision kwa kushirikiana na serikali mkoani Kagera, tayari limetoa jumla ya mifuko ya saruji 2300 yenye thamani ya shilingi milioni 39,000,000 kwa kaya 460 zilizobomolewa nyumba na zilizoonekana kuwa na uhitaji zaidi ambapo katika awamu ya kwanza kila kaya ilipaa mifuko mitano ya saruji na kwa sasa utekelezaji wa awamu ya pili umeanza ambapo inatarajiwa kugawiwa mifuko ya saruji 10,645 yenye thamani ya shilingi Milioni 164,997,000.00 kwa kaya 2,129.

Aidha tayari serikali imeainisha kaya nyingine zilizoathirika zaidi zipatazo 370 za watu waliomo kwenye makundi maalumu (Wazee, Wajane na Walemavu) ambao watapatiwa vifaa vya ujenzi (Mabati 20 na mifuko 5 ya saruji kwa kila kaya) kwa ajili ya kukarabati nyumba zao. Ugawaji kwa awamu ya kwanza umeanza.

HITIMISHO

Haya ndio niliyoyabaini katika ziara yangu nilipozuru Mkoani Kagera naishauri Serikali kuchukua hatua kali dhidi ya wale wate waliokuwa wanapotosha watanzania dhidi ya matumizi ya fedha hizi kwa makusudi kwa madai kwamba zimeliwa na serikali.

Lakini niwapongeze wananchi wote Mkoani Kagera ambao waliitikia wito wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuitikia wito wa kuanza ujenzi wa nyumba zao wao wenyewe huku serikali ikiunga mkono katika maeneo baadhi kama ambavyo nimeeleza katika makala yangu.

Jamii inapaswa kutambua kuwa hakuna serikali duniani ambayo inapanga Tetemeko la ardhi litokee ili liwauwe wananchi wake bali ni majanga ya asili ambayo kwa namna moja ama nyingine hayazuiliki.

Kwa wale wasomaji wa Biblia Takatifu Ukisoma Mathayo 3:2 inasema ”Tubuni, Kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribi” Nami nawasihi WATUBU wale wote waliokuwa wanapotosha kuwa hela za rambi rambi zimeliwa tena walipotosha bila kuwa hata na Data wala Taarifa sahihi za Matumizi ya fedha hizo.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger