Tuesday, 29 November 2016

SERIKALI YAKANUSHA KUHUSU WANAFUNZI WA DIPLOMA KUTOKWENDA DIGRII CHUO KIKUU

...

WIZARA ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi imetoa ufafanuzi kwamba haijapiga marufuku watu wenye Stashahada wenye sifa kujiunga na vyuo vikuu badala yake
walichokataza ni wanafunzi waliofeli kidato cha nne na cha sita kujiunga na vyuo vikuu bila kuwa na vyeti vyenye sifa.
Aidha, imesema kwa waliomaliza kupitia mfumo huo na wapo kazini ni wajibu wa waajiri wao kuhakikisha wana sifa za kazi wanazofanya na kutumia fursa hiyo kufanya mitihani ili kuwa na sifa zinazohitajika.
Naibu Waziri wa wizara hiyo, Stella Manyanya alitoa ufafanuzi huo jana Dar es Salaam kutokana na taarifa za upotoshaji zilizoenea mitandaoni kwamba serikali imepiga marufuku watu wenye Stashahada kujiunga na vyuo vikuu badala yake watakaoingia ni wenye sifa za kidato cha sita.
Manyanya alisema kwa waliopo vyuoni kwa sasa wanatakiwa kuhakikisha wanakuwa na sifa za shahada kwa kusafisha vyeti vyao na wapewe fursa ya kufanya mitihani hiyo waliyofeli na kama wamefaulu kozi hiyo, pia wataweza kufaulu mitihani hiyo itakayowapa sifa ya kusoma vyuo vikuu.
“Ni vitu tunavyovifanya wenyewe ila vina madhara makubwa, unakuta mtu anakaa nafasi kwa sababu ana vyeti, lakini uwezo hana… uhakiki utafanyika kwa vyeti na wanaofanya hivyo ni Utumishi,” alisema Naibu Waziri.
Alisema kwa watakaobainika pia kuingia vyuoni kwa sifa ambazo zilikuwa hazitakiwi kwa wakati huo ni batili zitafutwa na kwa watakaoingia kwa sasa vyuoni kwa kutumia njia zisizo rasmi na kubainika hata ikifika mwaka 2020 watafutwa kwa kuwa taarifa tayari wanayo.
“Kilichoongelewa siku ile ni kuruhusu kidato cha nne na kidato cha sita waliofeli kuingia kwenye ‘foundation course’ na diploma haikutajwa pale kwa kuwa haikuulizwa na hakuna kauli iliyotajwa pale kukataza watu wa diploma kwenda chuo kikuu,” alieleza Manyanya akirejea kauli ya Waziri wake, Profesa Joyce Ndalichako hivi karibuni katika mahafali ya Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT) yaliyofanyika mkoani Pwani.
Profesa Ndalichako alikaririwa akisema vigezo vya udahili vinatakiwa kuzingatiwa.
“Nami ningependa nizungumzie kwamba foundation course hazimuongezei mtu sifa. Kama sifa ya kujiunga na chuo kikuu ni kufaulu kidato cha sita, kama amefeli Baraza la Mitihani linaruhusu kurudia mtihani, kwa nini anakwepa kule? Kwa nini? Kwa nini tunataka tuendeleze uchochoro,” alieleza Waziri Ndalichako.
Naibu Waziri alisema kuna njia mbili za kwenda chuo kikuu ikiwemo njia ya moja kwa moja na njia ya mbadala ya kuwa na vyeti vinavyotambulika na kinasimamiwa na mamlaka husika ambayo ni Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) na wawe na ufaulu mzuri.
“Tanzania imejiwekea mifumo yake ya elimu ambayo inaendana na ngazi za kimataifa katika utoaji wa elimu na hapo awali tulikusudia kuhakikisha elimu inatolewa kwa watu wengi zaidi na hizo fursa zinawafikia wadau wote katika ngazi mbalimbali kwa kupanua elimu ya msingi hadi vyuo vikuu,” alieleza Naibu Waziri.
Alisema walitambua kuna wadau mbalimbali walitamani kusoma vyuo vikuu, lakini hawapati hiyo fursa na ndiyo wakaanzisha mfumo huo wa Chuo Kikuu Huria na mtu anaweza kusoma alipo na mfumo umekuwa ukiboreshwa siku hadi siku.
Alisema iliwekwa mifumo ya vyeti na ngazi zake kulingana na vigezo na hivyo siyo kila cheti kinachotolewa kinaruhusu mtu kwenda ngazi nyingine na kila mamlaka imepewa jukumu ili kulinda ubora wa elimu unaotolewa nchini.
Naibu Waziri alisema kutokana na uanzishwaji wa vyuo mbalimbali kumejitokeza changamoto na watu kutoka katika mfumo rasmi uliopangwa na kujiwekea mifumo binafsi ambayo imeingiza hata wanafunzi wa kidato cha nne ambao hawana sifa kuingia vyuo vikuu.
“Jambo hilo limesababisha kuwepo kwa msuguano, haiwezekani mtu afeli kidato cha nne bila kuwa na cheti kingine chochote anaingizwa katika kozi hiyo halafu anaingizwa chuo kikuu, sisi hatujarasimisha mfumo huo wa ‘foundation course’ na hatuna vipimo vyake,” alieleza.
Alisema kwa kawaida mwanafunzi mwenye diploma inayotambulika wamewekewa usawa wa alama fulani na kidato cha sita hivyo wanakuwa na sifa ya kuingia vyuo, lakini siyo waliofeli hivyo wanatakiwa kufanya utafiti zaidi katika kozi hiyo.
“Haiwezekani kila mtu akajianzishia mfumo wake tu, tulifikia eneo ambalo si zuri kama nchi na sasa tutaimarisha ubora…ukifeli kidato cha nne unatakiwa kwenda kusoma na kupata cheti kwenye mtaala unaotambulika na ukaenda diploma na unapofaulu unaweza kwenda chuo kikuu,” aliongeza.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Profesa Simon Msanjila alisema suala la ‘Foundation course’ limelenga kumuandaa mtu mwenye sifa ambaye amekuwa nje ya mfumo kwa muda mrefu ili kuingia chuo kikuu, lakini walichokuwa wakikifanya wengi ni kuwachukua waliofeli kidato cha nne na sita na kuwaingiza katika kozi hiyo na hatimaye kuwaingiza chuo kikuu.
Awali, baadhi ya wadau wa elimu nchini waliozungumza na gazeti hili wakiwemo wanataaluma walisema wanasubiri kupata taarifa rasmi kutoka wizarani kuhusu madai hayo, lakini wakaeleza manufaa ama athari za kutumika kwa mfumo huo nchini.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dares Salaam, Dk Benson Bana alisema haamini iliyonukuliwa ilikuwa kauli rasmi ya serikali, lakini akaongeza, “Upo utaratibu mbalimbali wa kuingia vyuoni na walio wengi wamepitia mfumo wa kuanzia cheti na kujiendeleza hadi kufika chuo kikuu na kutunukiwa digrii wakiwemo maprofesa na madaktari wengi.”
Alisema mfumo huo unasaidia kupata wanafunzi wengi wenye uzoefu na ambao huwasaidia wenzao katika kufanikisha elimu yao na huo ndio mfumo unaotakiwa.
Dk Bana alisema jambo linalotakiwa kutazamwa ni uwepo wa vyuo vingi vikuu ambavyo vimekuwa vikigawa alama za ajabu kwa wanafunzi, lakini wanapoingia vyuo mtihani ndio utakaowapembua.
Naye Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Ezekiah Oluoch alisema “Elimu ya kujiendeleza kuanzia ngazi ya cheti na kuendelea diploma, digrii na hata kufikia uzamivu ni mfumo uliopo dunia nzima.”
Alisema wapo wataalamu mbalimbali nchini na hata maprofesa ambao hawakusoma katika mfumo huo wakiwamo walimu wake (Ndalichako) waliosoma kupitia mfumo huo.
Imeandikwa na Hellen Mlacky, Lucy Lyatuu na Regina Kumba.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger