ZAIDI ya wanafunzi 200 waliodahiliwa katika Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom)
kwa mwaka (2016/17), wamelazimika kuacha masomo na kurejea nyumbani
baada ya kukosa mikopo ya elimu ya juu kutoka serikalini.
Imeelezwa kuwa wanafunzi hao wa mwaka wa kwanza walifika mapema chuoni
hapo kabla ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kutoa
majina ya wanufaika na wamefikia uamuzi huo baada ya bodi hiyo
’kuwatosa’ kutokana na kukosa sifa za kupata mikopo hiyo.
Aidha, zaidi ya wanafunzi 100 waliokuwa wanaendelea na masomo chuoni
hapo wamelazimika kusitisha kwa muda masomo yao kutokana na kuondolewa
kwenye orodha ya wanufaika kutokana na kubainika kuwa awali waliingizwa
kwenye orodha hiyo pasi na sifa za kupatiwa mikopo.
Saipulani Abubakar, waziri mkuu wa serikali ya wanafunzi chuoni hapo,
aliiambia Nipashe jana kuwa kutokana na kukosa mikopo kutoka HESLB,
wanafunzi hao wameshindwa kujilipia ada na kumudu gharama za maisha ya
chuo na wameamua kurudi nyumbani.
“Nusu ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza wameamua kurudi nyumbani kutokana
na kukosa mikopo kutoka serikalini, wengi ni watoto wa maskini,
wameshindwa kujilipia na kuamua kurudi nyumbani kufanya shughuli
zingine,” alisema Abubakar.
Alisema hadi mwishoni mwa wiki, ni wanafunzi wachache waliosajiliwa
chuoni hapo na hawafiki hata nusu ya waliodahiliwa kwa ajili ya mwaka
huu wa masomo.
Aidha, Abubakar alisema wapo wanafunzi wanaosubiri hatma yao kutokana na
HESLB kupeleka majina kwa mafungu katika vipindi tofauti chuoni hapo.
Alisema wanafunzi hao kwa sasa hawakai chuoni na wamekuwa wakiondoka na
kurejea chuoni kujua hatima yao.
Alibainisha kuwa miongoni mwa wanafunzi waliorudi nyumbani, wamo
waliopata asilimia ndogo ya mikopo ukilinganisha na ada wanazotakiwa
kulipa na hawana uwezo wa kumalizia kiasi kilichobaki.
Hata hivyo, kiongozi huyo wa wanafunzi alisema serikali yake iliangalia
vigezo vipya vilivyowekwa na bodi na kubaini kuwa baadhi ya wanafunzi
wanakidhi, lakini hawamo kwenye orodha ya wanufaika wa mikopo hiyo mwaka
huu.
Aliiomba serikali kuangalia upya mustakabali wa wanafunzi hao waliorudi nyumbani kwa kuwa wanapoteza ndoto zao.
“Ni kweli bodi iliweka vigezo vya wanafunzi kupata mikopo, lakini
tunashangaa kuona baadhi ya wanafunzi wenye sifa wanakosa, kuna
wanafunzi walisoma shule za kata, wengine hawana wazazi na wanaishi
vijijini ambako maisha ni magumu na wamenyimwa mikopo,” alisema.
"Wapo baadhi ya wanafunzi waliokosa mikopo hiyo, wakaamua kujilipia ada,
lakini kutokana na ugumu wa maisha hasa kukosa fedha kwa ajili ya
matumizi ya kawaida, wameamua kuahirisha mwaka ili wakajipange kwa ajili
ya mwaka ujao," aliongeza.
NUSU MWAKA
Alisema zaidi ya wanafunzi 100 waliokuwa wakiendelea na masomo lakini
waliokosa na kuamua kujilipia ada ya nusu mwaka, walifika ofisini kwake
kuandika barua za kuahirisha mwaka hadi pale hali ya maisha itavyokaa
vizuri na kuwapa fursa ya kuendelea na masomo.
Alisema kuwa kwa taarifa waliyopewa na HESLB, inaeleza kuwa wanafunzi
walioondolewa kwenye orodha ya wanufaika wa mikopo kwa mwaka huu wa
masomo licha ya awali kupewa, wamebainika kutumia vyeti feki vya vifo,
majina yao kutoonekana kwenye vitivyo wanavyopangwa na kutosaini
uthibitisho wa kupatiwa fedha.
Kiongozi huyo pia alibainisha kuwa kuna wanafunzi wanaondelea na masomo
lakini hawana uhakika kama wataendelea kunufaika na mikopo hiyo kwa kuwa
usajili kwa ajili ya mwaka huu wa masomo umesitishwa kusubiri HESLB
itoe majina ya wanafunzi inaoendelea kuwapa mikopo.
Kutokana na hali hiyo, Abubakar alisema serikali ya wanafunzi chuoni
hapo imeamua kukutana na Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi,
Teknolojia na Ufundi, Maimuna Tarish na Mkurugenzi wa HESLB, Abdul-
Razaq Badru, Novemba 20, mwaka huu kuzungumzia hatima ya wanafunzi
waliokosa mikopo.
Alipotafutwa na gazeti hili jana, Mkurugenzi Msaidizi wa Habari, Elimu
na Mawasiliano wa HESLB, Cosmas Mwaisobwa, alisema wanafunzi watakaopata
fedha mwaka huu ni wale waliokidhi vigezo vilivyowekwa.
Alisema bodi imefanya uchambuzi yakinifu wa kujua nani anastahili kupata mikopo hiyo na nani hastahili.
Mwaisobwa alisema bodi haiwezi kutoa msaada wowote kwa wanafunzi
waliokosa mikopo na kuamua kurejea nyumbani kwa kuwa kutokana na mfumo
wa kielektroniki uliotumika kufanya uchambuzi, imeweza kubaini wanafunzi
wenye sifa na wasio na sifa.
Mwaisobwa alisema “Sisi tunafuata sifa na vigezo vilivyowekwa vya utoaji
wa mikopo, hata kama wangerudi wote nyumbani, tunachoangalia ni vigezo
vya kupata huo mkopo”.
Alisema mwaka wa masomo 2016/17 Udom ulianza Oktoba 29, mwaka huu na
kwamba baadhi ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza waliobahatika kupata
mikopo, walipewa fedha kwa ajili ya chakula na malazi Ijumaa iliyopita.
Hivi karibuni, HESLB ilitangaza kuwaondoa zaidi ya wanafunzi 3,000
kwenye orodha ya waliotarajiwa kunufaika na mikopo hiyo kwa mwaka huu wa
masomo kutokana na kile ilichokielezwa kuwa ni kupungukiwa sifa.
Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru, alisema mbali na
kuondoa wanafunzi hao, wengine 87 ambao awali hawakujumuishwa kwenye
orodha ya wanufaika kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo kusoma shule
zisizo za serikali, sasa watapata mikopo baada ya kubainika walisomeshwa
na wafadhili.
Taarifa iliyotolewa na Badru Oktoba 30, ilibainisha sifa za wanufaika wa
mkopo kuwa ni wanafunzi yatima na walemavu, wanaotoka familia za hali
duni hususani waliosoma shule za umma na wale wanaosoma fani zilizo
kwenye kipaumbele cha taifa.
Fani hizo ni sayansi za tiba na afya, ualimu wa sayansi na hisabati, uhandisi wa viwanda, kilimo, mifugo, mafuta na gesi asilia.
Fani nyingine ni sayansi asili huku ya mwisho ikiwa ni sayansi ya ardhi, usanifu majengo na miundombinu.
Katika mwaka huu wa masomo, upangaji wa mikopo hiyo unazingatia bajeti
ya Sh. bilioni 483 zilizopitishwa na Bunge zikitarajiwa kunufaisha
wanafunzi 119,012, kati yao 25,717 wakiwa ni wa mwaka wa kwanza na
93,295 wanaoendelea na masomo yao.
0 comments:
Post a Comment