NAIBU Waziri wa Maji, Mheshimiwa Amos Makalla amegeuka mbogo kufuatia madai ya kukwepa kodi kupitia gari analodaiwa kulimiliki aina ya Toyota Dyna lililokamatwa na maofisa
wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wilayani Mvomero mkoani Morogoro hivi karibuni.
Naibu Waziri wa Maji, Mheshimiwa Amos Makalla
Akizungumzia habari zilizoandikwa na gazeti moja linalotoka kila siku
nchini kukanusha tuhuma hizo, Makalla alisema licha ya kuwa yeye siyo
mmiliki wa gari hilo lenye namba za usajili T534 BFP, lakini pia siku
lilipokamatwa, tayari lilishalipiwa leseni ya barabara.“Hizi ni mbinu chafu za kunichafua, siwezi kutoa misaada ya mamilioni kwa wapiga kura wangu halafu nikashindwa kulipa shilingi laki sita. Mimi siyo mmiliki wa hilo gari, ninaitwa Amos Gabriel Makalla, kadi ya gari imeandikwa Gabriel Amosi Makalla, wanajua siyo langu lakini wananichafua makusudi.
“Halafu kitu kingine ni kwamba gari lile limekaa gereji kwa muda mrefu sana na kwa sababu hiyo lisingeweza kulipa leseni ya barabara wakati halitembei, limekaa kule zaidi ya mwaka mzima. Hizi ni siasa za kuchafuana na hakika siwezi kukubali.
“Nimemuagiza mwanasheria wangu ashughulikie suala hili, habari hiyo siyo ya kweli, hainihusu na imelenga kunishushia heshima na kwa maana hiyo ninawadai kunilipa shilingi bilioni moja kwa sababu hadi wanaandika habari hiyo, gari hilo halikuwa linadaiwa,” alisema Makala.
0 comments:
Post a Comment