Watu
5 wamekufa papo hapo wakiwemo watu watatu wa familia moja na wengine 3
kujeruhiwa vibaya baada ya lori la kubebea mizingo kuparamia nyumba ya
kuuzia pombe katika kijiji cha Ugwachana, Manispaa ya Iringa.
Kamanda wa polisi mkoani humo,
Ramadhani Mungi, amesema ajali hiyo imetokea jana saa tatu usiku katika
kijiji hicho na Kitongoji cha Isimila katika Wilaya ya Iringa katika
barabara Kuu ya kutoka Iringa kwenda Mbeya.
Amesema
ajali hiyo imehusisha lori lenye namba T 878 AFB likiwa na trela
lililokuwa lenye namba T 570 AYY mali ya Kampuni ya MT Huwei ya mkoani
humo, lililokuwa linaendeshwa na Juma Omary (40), mkazi wa Makorongoni
na kuwa liliacha barabara na kuparamia Kilabu cha kunywea pombe ya
kienyeji na kuua watu hao wakiwa ndani ya kilabu hicho.
Amewataja
marehemu kuwa ni Leonard Mkendela (35), Neema Mkendela, na Kamsia
Mkendela, (wote wa familai moja) na wengine wawili ambao ni Mke na Mume,
Ester Mwalomo na Oscar Zosama (25) wote wakazi wa eneo hilo.
Hata
hivyo, amesema majeruhi wa ajali hiyo ni pamoja na dereva wa gari hilo,
Juma Omary (40), Musa Kadege (25), mkazi wa kijiweni, na Kasimu Mambo
(44) mkazi wa Kijiweni mkoani.
Amesema majeruhi hao wamelazwa katika
Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Iringa, na kuwa afya za watu wawili kati
yao wakiendelea vizuri na kuwa dereva wa gari hilo hali yake ni mbaya
ambapo amelazwa katika wodi ya wagonjwa mahututi (ICU).
0 comments:
Post a Comment