KUBADILISHA SHULE NA TAHASUSI KWA WANAFUNZI WA KIDATO CHA TANO 2014
Taarifa ya uchaguzi wa wanafunzi wa
kuingia kidato cha Tano katika Shule za Serikali na Vyuo vya Ufundi kwa
mwaka 2014 ilitangazwa kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI mwezi Juni,
2014. Wanafunzi waliochaguliwa awali walitakiwa kuripoti kuanzia tarehe
10 – 30/7/2014 .
Baada ya taarifa ya Uchaguzi wa wanafunzi
kutolewa, baadhi ya wanafunzi/wazazi/walezi wamewasilisha barua za
maombi ya kuwabadilishia wanafunzi waliochaguliwa shule na tahasusi au
mojawapo ya hivyo. Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI baada ya kupokea
imechambua maombi hayo na kubaini kuwa sababu zilizotolewa kwenye baadhi
ya maombi hayo zina tija na hivyo kulazimika kuridhia kuwabadilishia
shule, tahasusi au vyote kwa pamoja baadhi ya wanafunzi hao.
Hata hivyo, haikuwa rahisi kuwabadilishia
wanafunzi wote kulingana na uwasilishaji wa maombi yao kutokana na
ufinyu wa nafasi kwenye shule na baadhi ya wanafunzi kukosa sifa za
kubadilishiwa tahasusi kulingana na ufaulu walioupata. Kati ya maombi
3478 yaliyopokelewa na kuchambuliwa, wanafunzi 1518 (wavulana 759 na
wasichana 759) maombi yao yamekubaliwa na kubadilishiwa shule, tahasusi
au vyote kwa pamoja. Aidha, wanafunzi ambao hawataona majina yao
wafahamu kuwa maombi yao hayakufanikiwa, hivyo wanatakiwa kuripoti
kwenye shule walizopangiwa awali.
Hali kadhalika OWM – TAMISEMI
inawatangazia wanafunzi 320 wakiwemo wasichana 145 na wavulana 175 kuwa
wamechaguliwa kujiunga na shule mbalimbali za kidato cha tano, hali
iliyotokana na kuongezeka kwa nafasi katika baadhi ya shule.
Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI
inaendelea kutoa shukrani kwa ushirikiano wa wadau wa elimu na
inaendelea kuwasihi waendelee kutoa ushirikiano zaidi kwa ajili ya
kuboresha elimu nchini. Lengo ni moja la kufikia ufaulu wa asilimia 70
au zaidi kwa kidato cha nne wanaohitimu mwaka 2014 katika kufanikisha
malengo ya BRN tuliyojiweka. Aidha, naendelea kuwakumbusha jukumu
tulilonalo la kuongeza shule za sekondari za A – Level hususani zenye
miundombinu ya masomo ya sayansi ili kupata nafasi nyingi zaidi kwa
ajili ya kuwawezesha wanafunzi wote watakaofaulu kuingia kidato cha tano
mwaka 2015, wanapatiwa nafasi.
Aidha, wanafunzi wote ambao maombi yao yamekubaliwa wanatakiwa kuripoti shuleni si zaidi ya tarehe 30/7/2014 kama ilivyotangazwa awali.
BONYEZA HAPA CHINI KUANGALIA MAJINA HAYO
Imetolewa na Katibu Mkuu
OFISI YA WAZIRI MKUU – TAMISEMI
JULAI, 2014
0 comments:
Post a Comment