Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Samuel Sitta
Na Mwandishi wetu
15th July 2014
Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Samuel Sitta, kwa kushirikiana na Makamu Mwenyekiti, Samia Hassan Suluhu, wameteua wajumbe 30 wa Bunge hilo watakaoshiriki katika kikao cha kamati ya Mashauriano kitafachofanyika Julai 24 na 25 mwaka huu, katika ofisi ndogo za bunge jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwenye vyombo vya habari jana na Katibu wa Bunge hilo, Yahya Khamis, wajumbe wa kamati hiyo watafanya kazi ya kutathmini kazi ya bunge lao iliyokwisha kufanyika awali pamoja na ile itakayofanyika mwezi ujao.
Alisema uteuzi huo umefanyika chini ya masharti ya kanuni 54(4) na (5) za mwaka 2014.Aliwataja wajumbe walioteuliwa katika kamati hiyo kuwa ni pamoja na aliyekuwa Mwenyekiti wa muda wa Bunge hilo, Pandu Ameir Kificho, Profesa Costa Ricky Mahalu, James Mbatia, Freeman Mbowe, Ibrahim Lipumba, Peter Kuga Mziray, Vuai Ali Vuai, Askofu Donald Mtetemela, Sheikh Thabit Norman Jongo, na Job Ndugai.
Wengine ni Mwanasheria Mkuu wa serikali, Jaji Frederick Werema, Amon Anastaz Mpanju, Dk Francis Michael, Tundu Lissu, Margareth Abdallah, Kidawa Hamid Saleh,
Shamsi Vuai Nahodha, Abubakar Khamis Bakari, Dk. Asha Rose Migiro, na Othman Masoud Othman.Kadhalika, yupo Stephen Wasira, Hamad Rashid Mohamed, Askofu Amos Muhagachi, Susan Lyimo, Sheikh Hamid Masoud Jongo, Anne Kilango Malecela, Mary Pius Chatanda, Profesa Mark Mwandosya, Magdalena Sakaya na Khalifa Suleiman Khalifa.
CHIMBUKO LA MGOGORO
Aprili 16, mwaka huu wajumbe wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), waliusia kikao cha Bunge hilo kwa madai ya upendeleo na ubaguzi uliokuwa unafanywa na Chama Cha Mapinduzi dhidi ya vyama vingine.
Wajumbe hao wanaounda umoja huo kutoka vyama vya CUF, Chadema, NCCR-Mageuzi na wa vyama vingine, walichukua hatua hiyo pia wakituhumu kauli ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, waliyodai kuwa ni za ubaguzi na vitisho akiwa kanisani kwamba Wazanzibari wanaotaka serikali tatu wanataka ijitenge ili iwe nchi ya Kiislamu.
Msimamo huo ulitolewa siku hiyo jioni na Profesa Ibrahim Lipumba alisema kuwa Lukuvi alitoa kauli hiyo mkoani Dodoma katika Kanisa la Methodist wakati wa sherehe za kumsimika Askofu Joseph Bundara wa Jimbo la Dodoma.
Profesa Lipumba alisema kwamba Lukuvi aliyemwakiisha Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alizungumza lugha ya vitisho ndani ya kanisa kwamba kama serikali tatu zitaundwa na serikali ya Muungano ikashindwa kuwalipa mshahara wanajeshi, Jeshi litachukua nchi.
Alisema kuwa kauli hizo zilisababisha Askofu Bundara kusema kwamba ni vema Katiba ya Zanzibar ikafutwa na kuundwa katiba moja.
Lipumba alisema Bunge limegeuka kuwa Interahamwe akimaanisha wanamgambo waliochochea ubaguzi na kusababisha mauaji ya kimbari nchini Rwanda mwaka 1994.
“Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni muumini ya dini ya mwenyezi Mungu, lakini naafiki mapendekezo yaliyoletwa kwetu na Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambayo ni Tume iliyoundwa na Rais.
UBAGUZI
“Na waziri Lukuvi alikuwa anamwakilisha Waziri Mkuu, Mizengo Pinda…Mheshimiwa hii inasikitisha na inasikitisha kwa kuwa kauli hii pia inafanana na kauli ambayo Rais Jakaya Kikwete aliitoa wakati akitoa hotuba katika bunge hili,” alisema.
“Hii ni Rasimu ya Tume ya Rais na si rasimu ya Wapemba, lakini katika mjadala wetu hapa umekuwa na utaratibu wa ubaguzi, watu wamebaguliwa humu na viongozi wakubwa wanapiga makofi, Bunge hili limekuwa kama Bunge la ‘Intarahamwe’, hii ni hatari kwa nchi yetu,
“Wapemba, Waarabu, Wahindi, Wakongo, hii hatuitaji katika nchi yetu, tunahitaji katiba ambayo itahakikisha kila mwananchi anapata haki yake wote tuwe sawa, bila kujali, rangi zetu, makabila yetu, dini zetu, hii ndiyo nchi aliyotuachia Mwalimu Nyerere,” alisema.
“Kutokana na hali hii, tumechoka kusikiliza matusi, tumechoka kudharau mawazo ya wananchi, tumechoka ubaguzi, hatuwezi kuwa sehemu ya kundi la Interahamwe linalohamasisha ubaguzi ndani ya Tanzania…hili hatulikubali, hatulikubali, tunawaachia, watu wote tunaotaka katiba ya wananchi tunawaachia Interahamwe muendelee na kikao chenu,” alisema.
“Hatuwezi kuwa sehemu ya Interahamwe,” alisema Profesa Lipumba na baada ya kumaliza kuzungumza, wajumbe wote wa Ukawa na wengine walisimama na kuondoka ndani ya ukumbi huku wakipiga kelele.
Baada ya kutoka nje ya ukumbi wa Bunge huku wajumbe wa kundi hilo linalojumuisha vyama vya hivyo pamoja na NLD kinachoongozwa na Dk. Emmanuel Makaidi, DP kinachoongozwa na Mchungaji Christopher Mtikila na baadhi ya wajumbe wa kundi la 201, huku wakiimba nyimbo mbalimbali. “Tunaondoka, tunawaacha Interahamwe, Interahamwe.”
LUKUVI NA KANISA
Alitaja sababu nyingine iliyowafanya watoke nje ya ukumbi wa Bunge wakati mjadala ukiendelea ni hatua ya Lukuvi kuzungumza ndani ya kanisa, akieleza kuwa ulikuwa ni makakti maalum wa kuwabana Wazanzibari.
Profesa Lipumba aliwataka wajumbe hao kuhudhuria kikao cha pamoja kitakachofanyika leo kwa ajili ya kuweka mikakati ya nini cha kufanya.
TUTARUDI IWAPO…
Baada ya kikao hicho, Prof. Lipumba alipoulizwa na waandishi wa habari kama Ukawa wamesusia moja kwa moja Bunge la Katiba, alisema wanaweza kurudi endapo tu mambo yatakayokuwa yakijadiliwa ni yale tu yaliyomo katika Rasimu iliyopendekezwa na Tume ukiwamo muundo wa Muungano wa serikali tatu.
MADHARA KWA THELUTHI MBILI
Ikiwa hawatarejea bungeni wataathiri upitishaji wa katiba kwa sababu kanuni namba 36 (1) bila kuathiri masharti ya sheria na kanuni hizi, mapendekezo ya marekebisho, au mabadiliko yaliokidhi matakwa ya na masharti ya kanuni hizi kuhusu sura za rasimu ya katiba zinazohusika yatajadiliwa na kupigiwa kura ibara kwa ibara katika kipindi kisichozidi siku moja.
Ibara ya 2 inasema mapendekezo ya marekebisho au mabadiliko yaliyowasilishwa kwa mujibu wa fasiri ya (1) yatapigiwa kura na kupitishwa kwa kuungwa mkono kwa wingi wa theluthi mbili ya wajumbe wote kutoka Tanzania Bara na theluthi mbili ya wajumbe wote kutoka Tanzania Zanzibar.
Ibara ya 3 inasema pale mapendekezo ya marekebisho, maboresho au mabadiliko yatakubaliwa, ibara inayohusika ya rasimu ya katiba itahesabiwa kuwa imepitishwa pamoja na mabadiliko yake isipokuwa kwamba pale ambako mapendekezo ya marekebisho, maboresho au mabadiliko yatakataliwa, ibara inayohusika ya rasimu ya katiba itapigiwa kama ilivyokuwa kwa kufuata masharti ya fasiri ya (2).
Ibara ya Nne, endapo baada ya kupigiwa kura, theluthi mbili ya wajumbe wote kutoka Tanzania Bara na theluthi mbili ya wajumbe wote kutoka Tanzania Zanzibar haikufikiwa, basi ibara hiyo itapelekwa kwenye kamati ya mashauriano ili kupata muafaka.
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, inawatambua wajumbe wote waliokula kiapo na ndiyo sababu baadhi ya kamati miongoni mwa 12, zilizochambua rasimu zilishindwa kupitisha maamuzi kutokana na kukosa theluthi kwa pande zote wakati wa kupiga kura kutokana na baadhi ya wajumbe kutokuwapo.
CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment