Alexander Msowoya (35), ambaye ni mkazi wa Chang’ombe, jijini Dar es Salaam, amefikishwa katika Mahakama ya Mwanzo Magomeni akikabiliwa na shtaka la kumteka nyara askari wa kike wa usalama barabarani.
Akiwa anaendesha gari, mshtakiwa huyo anadaiwa kumteka Kostebo Ester
katikati ya maeneo ya Tameke na Chang’ombe kabla ya kukamatwa maeneo ya
katikati ya Mabibo na Ubungo baada ya msako mkali wa polisi waliokuwa
wakitumia redio za upepo.
Hati ya mashtaka iliyosomwa mbele ya hakimu Mwanaidi Ngoda ilidai kuwa
Julai 11, mwaka huu, saa 9:00 alasiri, eneo la kati ya Temeke na
Chang’ombe, mshtakiwa alimteka nyara askari polisi Konstebo Ester,
alipotakiwa kuonyesha leseni yake.
Ilidaiwa kuwa Afande Ester alimkamata mshtakiwa huyo akiwa anaendesha
gari lenye namba za usajili T 495 BKJ na kumtaka aonyeshe leseni yake,
lakini hakufanya hivyo.
Baada ya hapo, ikadaiwa kuwa trafiki huyo wa kike akamwamuru dereva huyo
aliyekuwa anaendesha gari aina ya Rav4 ya rangi ya bluu kuweka gari
lake pembeni, lakini alikaidi kwa kudai ana haraka.
Kutokana na hali hiyo, ilidaiwa kuwa askari aliingia ndani ya gari kwa
kupitia kwenye mlango wa nyuma na kuamuru waende kwenye kituo cha polisi
Chang’ombe.
Hata hivyo, ilidaiwa kuwa badala ya kuelekea alikoelekezwa, mshtakiwa
alianza kwenda anakokujua yeye, hivyo kukiuka amri halali ya polisi na
kitendo hicho kuhesabika kama ni utekaji nyara.
Awali, kabla ya kesi hiyo kusomwa, askari polisi mmoja alimwambia
mwandishi wa habari hizi kuwa kilichomuokoa afande Ester ni redio ya
mawasiliano aliyokuwa nayo, ambayo kwa kiasi kikubwa ilifanikisha kujua
walipo na wanakoelekea.
Hivyo, walikuwa wakifanya mawasiliano na askari wengine waliokuwa maeneo mbalimbali gari linapopita na ikasaidia kukamatwa.
“Afande amepumzika nyumbani kwake. Kwa sasa hali yake si nzuri ana
presha kutokana na tukio hili,” alisema askari mmoja wa kiume mahakamani
hapo, ambaye hakutaka kutaja jina lake.
Hata hivyo, alidokeza kuwa kuna uwezekano mkubwa kesi hiyo ikapelekwa
kwenye mahakama za juu kutokana na uzito wake, kwani ni ya utekaji
nyara.
Mshtakiwa alikana shtaka hilo na kupelekwa rumande. Kesi hiyo imepangwa kuendelea tena Julai 27, mwaka huu.
0 comments:
Post a Comment