Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga SAC Justus Kamugisha akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo mchana |
Siku
moja tu baada ya abiria 63 kunusurika kufa baada ya basi la
Supernajimunisa lilikitoka Mwanza kwenda Dar es salaam kupinduka huko
Usanda Shinyanga,leo
wafanyabiashara watatu wamefariki dunia na wengine 46 kujeruhiwa baada ya lori aina
ya Fuso walilokuwa wanasafiri na bidhaa zao kuacha njia na kupinduka katika kijiji cha Uchunga wilayani Kishapu.
Ajali hiyo imetokea leo saa
tatu asubuhi baada ya lori lenye namba za usajili T680 ARL aina ya Fuso lililokuwa
limepakiza mizigo na wafanyabiashara ambao idadi yao bado haijajulikana likitokea kijiji cha Kiloleli wilayani Kishapu
kwenda katika mnada wa Mhunze uliopo Kishapu.
Kamanda wa
polisi mkoa wa Shinyanga Justus Kamugisha amesema katika taarifa za awali
ajali hiyo imetokana na mwendo kasi wa gari gari
hilo aina ya fuso mali ya Ngasa Seni mkazi wa Kiloleli lililokuwa
likiendeshwa na Shija Ngasa mfanyabiashara ,mkazi wa Kiloleli wilayani
Kishapu ambalo lilimshinda dereva na kuacha
njia kisha kupinduka na kusababisha vifo na majeruhi.
“Hili gari ni lori linatumika kubeba mizigo lakini,lilikuwa limepakiza abiria ,wengi ni wafanyabiashara,lilikuwa linatoka Kiloleli kwenda Mhunze mnadani,liliacha njia na kupinduka,dereva alitoroka baada ya kutokea ajali hiyo na anatafutwa na jeshi la polisi.
Watu
waliopoteza maisha mpaka sasa ni watatu,majeruhi 46, 35 na wanapata
matibabu katika hospitali ya mkoa wa Shinyanga na 11 katika hospitali ya
Kolandoto,japokuwa kuna taarifa kuwa majeruhi wanaweza kuongezeka kwani
wengine walipelekwa Kishapu.
Kamanda
Kamugisha ametoa wito kwa wamiliki wa magari,wananchi wakiwemo wafanyabiashara
kuacha tabia ya kutumia magari yasiyo ya abiria kusafiria.
Amewashauri
wafanyabiashara kubadilika na kuacha ubahiri wa kupenda vitu rahisi
hivyo wawe wanapanda magari ya abiria badala ya kupanda magari ya
mizigo.
Kaimu
mganga mfawidhi wa
hospitali ya mkoa wa Shinyanga Dkt Maguja Daniel amesema wamepokea miili
miwili
ya marehemu na mwingine mmoja alifariki wakati akipatiwa matibabu na
majeruhi 35 na wanaendelea kupatiwa matibabu katika hospitali hiyo.
0 comments:
Post a Comment