WAZIRI Mkuu wa
zamani, Frederick Sumaye, amewashukia wale wanaotumia kete ya umri
kuwania urais na kwamba, hawafai kuwa viongozi wa taifa la Tanzania.
Kauli hiyo,
inaonekana ni kujibu mapigo ya Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia, January Makamba (40), ya kuwataka wazee wakae pembeni na
kuwachia vijana kuwania urais katika uchaguzi mkuu ujao.
Sumaye, aliyasema hayo jana wakati akihojiwa na kituoa cha runinga cha Star cha jijini Mwanza jana.
“Nakumbuka mwaka
2005 wakati Rais Jakaya Kikwete hajawa Rais, akigombea nafasi hiyo
kulitawala msemo huo wa kumtaka kwa turufu ya kusema ni kijana, huku
wakati huo alikuwa na miaka 55, wengine tukawa tunajiuliza hivi, kumbe
mwenye miaka 55 ni kijana,” alihoji Sumaye.
Alibainisha kuwa,
kwa kufuata misingi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), hafikirii kama kuna
kijana hata mmoja ambaye ana sifa ya kuwa Rais, kwani chama hicho
kinamtambua kijana ni yule mwenye miaka 18 hadi 35.
“Kwa misingi hiyo,
sijajua kama kijana anayemaanishwa kwa sasa ni huyo au mtu mzima ambaye
hajazeeka, hivyo kwa maoni yangu kiongozi anayetufaa ni mtu tunayemuona
ana nguvu, muadilifu, mchapakazi na anayetaka kutuongoza na sisi tunaona
anatufaa, bila kujali kama ni kijana, mwanamke, mlemavu au ni wa dini
gani, anatoka wapi, ili mradi ni mtanzania, kwa dhamira ya wazi huyo
atatusogeza mbele na ndiye tutakayemtaka na si kwa sababu ya ujana au
uzee wake,” alisema.
Sumaye, alimnukuu
Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere kuwa, aliwahi kuzungumzia suala hilo
wakati lilipojitokeza katika chaguzi zilizopita akisema; “Ujana si sifa,
nani hajawahi kuwa kijana?’.
Sumaye alisema, ujana ni hatua ya binadamu ya kukua na haiwezi kuwa sifa ya urais, kwani sifa ni tofauti na ujana.
“Simaanishi kwamba
vijana hawafai kuwa viongozi, ila kama yupo anayefikiria kwa maana
anaitwa ‘fulani fulani’ anaona ana uwezo wa kuendesha hii nchi na watu
wakakubali kwamba anao uwezo, ni muadilifu, anajua matatizo ya
Watanzania na atasimamia maslahi ya umma, tutamchagua, lakini asiende
pale kwa kigezo cha kwamba yeye ni kijana, kwa sababu hiyo si miongoni
mwa sifa za uongozi na ukitaka uongozi kwa misingi hiyo, utakuwa
hutufai,” alisema Sumaye.
Akizungumzia kuhusu
nafasi za uongozi kwa vijana, Sumaye alisema kuwa, wapo wanaoshika
nyadhifa mbalimbali ikiwamo bungeni, ukuu wa wilaya na hata kwenye
vyama, kuna timu ya vijana wengi, hivyo kama wanania ya kubadilisha nchi
wanaweza kubadili kwa kupitia nafasi hizo.
“Naamini vijana
wengi hawakupewa uongozi serikalini, ukiachilia wale wa nafasi za
uwakilishi wa vijana wanaoingia bungeni kwa kufuata sheria ya CCM,
lakini kama mkuu wa Wilaya, Rais humteua kwa uwezo na si ujana wake, kwa
hiyo suala la ujana au uzee lisitupotezee muda, kwa sababu lina nia ya
kutuondoa kwenye ajenda bila sababu.
“Natoa wito kwa
Watanzania tusiyumbishwe ili tuweze kumchagua Rais tunayemtaka bila ya
kujali sifa za ujana, udini na jinsia, kwani si moja wapo ya sifa
zinazotakiwa kwa rais anayetufaa,” alisema Sumaye.
Akifafanua madai
kwamba wazee wamekuwa wakiwabana vijana kuchukua nafasi za juu, Sumaye
alisema, hilo halina ukweli kwa sababu katika ngazi za Chama Cha
Mapinduzi, zipo Jumuiya za Vijana ambazo zinatoa nafasi pana kwa kuwapa
uwakilishi.
“Naamini iwapo
vijana wanataka kuleta mabadiliko, hakuna wa kuwazuia, kwani tangu
nimekuwa ndani ya chama hakuna hoja yoyote ya mabadiliko iliyotolewa na
vijana ikapingwa na wazee,” alisema.
Kauli hiyo ya
Sumaye, imekuja baada ya hivi karibuni, January kutangaza nia ya kuwania
urais huku akitoa wito wa kuwataka wazee kukaa pembeni ili vijana
walete mabadiliko chanya ya uongozi.
January alisema
kuwa, ameamua kwa asilimia 90 kujitokeza kuwania urais katika uchaguzi
mkuu wa mwaka 2015 na asilimia zilizobaki zitategemea mambo mengine.
Katika ukurasa wake
kwenye mitandao ya kijamii wa Facebook na Twitter, January alisema,
uongozi wa kizazi kipya upo tayari kushika hatamu za uongozi na kuijenga
Tanzania mpya, fikra mpya na maarifa mapya.
Alisema, mabadiliko
yaliyotokea Tanzania, yalidaiwa na kuongozwa na vijana na kwamba,
vijana nchini wanaweza kushika usukani wa kuleta mabadiliko
wanayoyataka.
“Ukiona kijana
anamwambia kijana mwenzake hana uzoefu, basi kazi ya kuleta mabadiliko
ni kubwa zaidi na kutokuwa na uzoefu ni sifa ya kijana,” aliandika.
Alisema kuwa, tusi
kubwa kwa Rais wa Marekani, Barack Obama mwaka 2008, lilikuwa ni kukosa
uzoefu na kukosa rekodi, lakini tusi hilo liligeuka kuwa muziki kwa
wapiga kura wa nchi hiyo.
“Tanzania mpya
inahitaji viongozi wapya, mazoea mapya, fikra mpya na maarifa mapya.
Inahitaji kuthubutu mambo makubwa, siyo kulinda uzoefu wa nyuma,”
aliandika January.
0 comments:
Post a Comment