MAMLAKA
ya Kupambana na Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA), imemhoji
Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, baada
ya kuwahusisha baadhi ya viongozi na watendaji wa Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar na tuhuma za ufisadi.
Ofisa
wa Kitengo cha Elimu kwa Umma cha ZAECA, Abubakari Mohamed Lunda,
alisema jana kuwa Maalim Seif alihojiwa na Mkurugenzi wa ZAEC, Mussa
Haji Ali, ili athibitishe tuhuma hizo.
Lunda
alisema tuhuma zilizotolewa dhidi ya watendaji na viongozi ni nzito
ndiyo maana mamlaka hiyo imeamua kuchunguza ukweli wake kwa manufaa ya
Zanzibar na wananchi wake.
Lunda
alisema kazi kubwa ya mamlaka hiyo ni kuchunguza jambo lolote ambalo
linahusu maslahi ya Zanzibar katika kupambana na vitendo vya rushwa na
uhujumu uchumi.
“Tayari
mamlaka imemhoji Maalim Seif ili kutafuta ukweli juu ya tuhuma alizotoa
za kuwapo viongozi wanaomiliki fedha chafu na mali nje ya nchi,” alieleza Lunda.
Alisema
nia ya kumhoji Maalim Seif ilikuwa kupata ukweli wa tuhuma alizotoa
dhidi ya viongozi na watendaji aliowatuhumu kwa kumiliki fedha chafu na
mali nje ya nchi.
Hata
hivyo, Lunda alisema mpaka sasa hafahamu mkurugenzi amegundua kitu gani
baada ya kufanyika kwa mahojiano hayo huku akisisitiza kuwa ZAECA
imetimiza wajibu wake wa kupokea na kuchunguza taarifa mbalimbali
wanazopata kupitia wanasiasa, vyombo vya habari na wananchi.
Lunda
pia alisema kuna majalada 20 yamekabidhiwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka
Zanzibar (DPP), Ibrahim Mzee kwa ajili ya hatua za kisheria kuchukuliwa.
Alisema
majalada hayo yanahusisha kesi mbalimbali zikiwamo za rushwa ya
uchaguzi zilizotokea wakati wa kura ya maoni ya kuwapata wagombea wa
ubunge na uwakilishi kupitia CCM mwaka jana.
Alisema
kitendo cha majalada kukaa muda mrefu kwa DPP bila ya kufunguliwa
mashtaka mahakamani si jukumu la ZAECA kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar
ya Mwaka 1984.
"Ni jukumu la Mkurugenzi wa Mashtaka wa Zanzibar (DPP)," alisema.
Akizungumza
na waandishi wa habari, Aprili 10 mwaka huu mjini Zanzibar, Maalim
Seif, ambaye ni Makamu wa kwanza wa Rais wa zamani wa Zanzibar alituhumu
kuna viongozi na watendaji wa visiwani humo wanamiliki fedha chafu na
mali nje ya nchi.
Alisema
kuwa fedha hizo zilipatikana kwa njia za ufisadi na kutaka jumuiya ya
kimataifa kufuatilia akaunti za vigogo hao na watendaji nje ya nchi kwa
manufaa ya Zanzibar na wananchi wake.
Maalim
Seif alidai kuwa haihitajiki tochi kuwamulika viongozi wanaokabiliwa na
tuhuma za ufisadi na kutaka mamlaka za dola kufanya uchunguzi dhidi ya
vigogo hao na kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria.
0 comments:
Post a Comment