WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema Taifa limepoteza kijana aliyekuwa msatari wa mbele kuwahamasisha vijana wajitambue wawe wazalendo kwa nchi yao na watambue fursa za maendeleo zilizopo na wasiwe walalamikaji.
Ameyasema hayo leo (Jumatano, Februari 27, alipokwenda kuhani msiba wa aliyekuwa Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji wa Clouds Media Group, Ruge Mutahaba kwa niaba ya Serikali, nyumbani kwa wazazi wa marehemu Mikocheni jijini Dar es Salaam.
Waziri Mkuu amesema vijana nchini walikuwa na kiongozi aliyekuwa akiwaongoza kwa kuwafungua kimawazo na kuwaonesha fursa mbalimbali zitakazowawezesha kuwakwamua kifikra na kiuchumi ili waweze kujitegemea.
Waziri Mkuu amesema msiba huo ni wa wote kwani marehemu amefanya kazi kubwa ya kushirikiana na Serikali kuhamasisha vijana kujitambua na kutambua fursa zilizpo na kuzifanyia kazi. “Ruge ametoa mchango mkubwa kwa Taifa
Amesema marehemu Ruge katika kipindi cha uhai wake amefanya kazi kubwa kwa upande wa Serikali, kuanzia awamu ya nne hadi ya tano hususani katika suala la kuhamasisha vijana kujikwamua na kutokuwa wategemezi.
Pia, Waziri Mkuu amesema historia yake inaeleza namna alivyozunguka nchi nzima na kukutana na makundi ya vijana mbalimbali na kuwaelimisha namna ya kutambua fursa zilizopo nchini huku akiwahamasisha wawe wazalendo.
"Marehemu alikuwa akitoa hadi fedha zake binafsi kwa ajili ya kuwawezesha vijana hasa wale ambao hawakuwa na uwezo wa kiuchumi ili nao washiriki katika shughuli mbalimbali za ujasiriamali na hatimaye waondokane na utegemezi.”
Kadhalika, Waziri Mkuu ametoa wito kwa wazazi, watoto wa marehemu pamoja na wananchi kwa ujumla waendelee kuwa na subira na watulivu katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na mpendwa wao.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATANO, FEBRUARI 27, 2019.
0 comments:
Post a Comment