Baadhi ya watuhumiwa nane waliohukumiwa kifungo cha maisha kwa kosa la kuchoma moto kituo cha polisi.
Wakili wa kujitegemea nchini Jebra Kambole amebainisha kusudio la kuwakatia rufaa baadhi ya waliohukumiwa kifungo cha maisha kwa kukutwa na hatia ya makosa 6 ikiwemo kuchoma moto kituo cha polisi Bunju A Jijini Dar es Salaam.
Licha ya Jebra Kambole, mawakili wengine watano wanakusudia kukata rufani kupinga hukumu ya kifungo cha maisha jela iliyotolewa wiki iliyopita na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, dhidi ya washtakiwa wanane.
Akizungumzia uamuzi huo Wakili Jebra Kambole amesema "kwa sasa tumeshatoa notisi ya kusudio la kukata rufani maana kikawaida inatakiwa utoe notisi ndani ya siku 10, baada ya hapo, utaratibu mwingine utafuata".
Mbali na kosa la kuchoma moto kituo cha polisi, vijana hao walihukumiwa kwa makosa sita yakiwamo ya kufanya mkusanyiko usio halali, kuharibu mali, kumwagia petroli na kuchoma moto Kituo cha Polisi cha Bunju A, mwaka 2015.
Awali kesi hiyo ilikuwa na washtakiwa 35, lakini baadaye Mahakama iliwaachia huru washtakiwa 17 na kati ya 18 waliobakia, wanane ndiyo walitiwa hatiani Ijumaa iliyopita, huku 10 wakiachiwa huru.
Waliokutwa na hatia na kuhukumiwa kifungo cha maisha ni Ramadhan Said (22), Veronica Ephraim (32), Yusuph Sugu (40), Juma Kozo (32), Rashid Liwima (29), Baraka Nkoko (23), Abuu Issa (36) na Abraham Mninga (23).
0 comments:
Post a Comment