Mzee Musa Katambo, baba mzazi wa Ally Katambo (30), ambaye amehukumiwa kwenda jela miaka 30 baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara kumkuta na hatia ya kumbaka mtoto wake wa kumzaa mwenye umri wa miaka 11, amefurahia kifungo cha mwanawe.
Ally alitiwa hatiani na kupewa adhabu hiyo kutokana na kumfanyia binti yake huyo mwanafunzi wa darasa la nne kitendo cha kinyama.
Mzee huyo alishangilia na kuipongeza mahakama kwa kutoa hukumu hiyo ya kifungo cha miaka 30 jela dhidi ya mwanae, akisema kosa alilolifanya la ubakaji ni kinyume cha sheria za nchi.
Katambo ambaye anaishi kijijini kwake Ndanda wilayani Masasi Mkoani Mtwara, alisema kwamba hajutii maamuzi ya mahakama dhidi ya mtoto wake huyo kufungwa miaka 30 jela, na kwamba serikali imetenda haki katika kusimamia sheria hasa juu ya vitendo vya ukatili dhidi ya watoto.
Mzee Katambo aliyasema hayo mwishoni mwa wiki alipokuwa akizungumza na gazeti hili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Masasi, baada ya mtoto wake huyo kuuhukumiwa kwenda jela miaka 30.
Alisema amefurahishwa na hukumu hiyo kwa sababu itatoa fundisho kwa vijana wengine wenye tabia kama ya mtoto wake kwa kuwa watakaposikia wataacha kufanya vitendo hivyo, ambavyo vinaonekana kuchochewa na imani za kishirikina, badala yake vijana wafanye kazi kwa bidii ili waweze kutimiza ndoto zao.
Alisema serikali ya sasa inasimamia haki kuhusiana na vitendo vya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto hasa pale wanapofanyiwa vitendo hivyo na wazazi wao.
Alisema kitendo alichofanya mtoto wake dhidi ya mjukuu wake ni cha kikatili na kimeiletea aibu familia yake.
“Kwa kweli enzi zetu sisi yaani ile miaka ya zamani hakukuwa na mambo kama haya ya ajabu, mzazi kumbaka mwanawe wa kumzaa kisa kaambiwa na mganga ili apate utajiri,” alisema na kuongeza:
“Mambo kama haya sisi ndio kwanza tunayaona siku hizi zamani hayakuwapo kabisa kwa hili mimi naipongeza serikali imetenda haki kabisa.”
Mzee Katembo alisema siku ya kwanza alipopata taarifa ya kuwa mjukuu wake amebakwa na baba yake mzazi na binti huyo kulazwa katika hospitali ya Mision ya Ndanda mjini Masasi, alipoteza fahamu kwa vile katika maisha yake hakuwahi kusikia jambo kama hilo la baba kumbaka mtoto wake wa kumzaa.
Aliongeza kuwa hata alipokuwa akifunga safari ya kwenda hospitalini Ndanda kwa ajili ya kumuona mjukuu wake anaendeleaje baada ya kulazwa pia alipokuwa akiingia ndani ya hospitali hiyo, alikuwa akianguka na kupoteza fahamu kwa mara mbili mpaka tatu ndipo anapata fahamu.
Na Hamisi Nasiri - Nipashe
0 comments:
Post a Comment