Monday, 25 February 2019

MAHAKAMA YAKATAA KUTOA HATI YA KUMKAMATA TUNDU LISSU

...
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, imekataa kutoa hati ya kumkamata mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, kutokana na wadhamini wake kufika mahakamani hapo na kueleza hali halisi ya matatizo yake.

Pia, Mahakama hiyo imewaonya wadhamini wa mshtakiwa huyo kuhakikisha kuwa wanafika mahakamani hapo kila kesi hiyo inapotajwa.

Uamuzi huo umefikiwa leo Jumatatu, Februari 25, 2019 na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, baada ya upande wa mashtaka kuiomba mahakama hiyo itoe hati ya kumkamata Lissu kwa sababu anazunguka nchi mbalimbali kutoa mihadhara.

"Hati ya kumkamata mshtakiwa kwa sasa haiwezi kutolewa, hivyo nawaonya wadhamini kufika mahakamani kila kesi hii inapotajwa" amesema Hakimu Simba.

Awali, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon amedai mahakamani hapo kuwa shauri hilo lilikuja kwa ajili ya kutajwa.

Simon amedai Februari 4, 2019, mahakama hiyo iliamuru wadhamini wa Lisu kufika mahakamani hapo kueleza hali ya mbunge huyo kwa kuwa Mahakama hiyo haina rekodi ya taarifa zaidi ya kusikia na kuona katika luninga.

"Kama itakupendeza mheshimiwa hakimu tunaiomba mahakama yako itoe hati ya kumkamata mshtakiwa kwa kuwa tunamuona anazunguka nchi mbalimbali kufanya mihadhara," amedai Simon.

Baada ya Wankyo kueleza hayo, Hakimu Simba amesema hati ya kumkamata mshtakiwa kwa sasa haiwezi kutolewa na mahakama hiyo.

Pia, Hakimu Simba amewataka wadhamini wa Lissu ambao ni Ibrahim Ahmed na Robert Katula kuhakikisha wanahudhuria mahakamani hapo kila kesi hiyo inapokuwa Inatajwa.

Hakimu Simba ameahirisha kesi hiyo hadi Machi 25, Mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.

Kesi hiyo ipo katika hatua ya usikilizwaji wa ushahidi wa upande wa mashtaka, lakini imeshindwa kuendelea kutokana na mshtakiwa wa nne katika kesi hiyo, ( Lissu )kuwa nchini Ubeljiji kwa ajili ya matibabu.

Mbali na Lissu, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni wahariri wa Gazeti la Mawio, Simon Mkina na Jabir Idrisa na Mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehbooh.

Kwa pamoja washtakiwa hao, wanakabiliwa na mashtaka matano likiwamo la kuandika habari za uchochezi kinyume na Sheria ya Magazeti ya Mwaka 2002.

Wanadaiwa kutenda makosa hayo kati Januari 12 na 14, 2016 jijini Dar es Salaam, ambapo Jabir, Mkina na Lissu, waliandika na kuchapisha taarifa za uchochezi zenye kichwa cha habari kisemacho, ‘Machafuko yaja Zanzibar.’

Katika shtaka la pili wanadaiwa kuwa Januari 14, 2016 walichapisha habari hizo ili kuleta chuki kwa wananchi.

Na Hadija Jumanne, Mwananchi 
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger