NA TIGANYA VINCENT
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan amewataka wafanyabiashara wadogo kulipia na kuchukua vitambulisho maalumu vilivyotolewa na Serikali kwa ajili yao vinginevyo vitahesabika kuwa ni wafanyabiashara wakubwa wanaopaswa kulipia kodi.
Hatua itasaidia kuwatambua na kuepusha usumbufu wakati wa kufanya shughuli zao za kujiletea maendeleo.
Makamu wa Rais alitoa kauli hiyo kwenye mkutano wa hadhara katika uwanja wa TASAF wilayani Sikonge ikiwa ni siku tatu ya ziara yake mkoani Tabora .
Alisema mfanyabiashara ndogo ndogo asiyetaka kulipia shilingi 20,000/- za kitambulisho maalumu atahesabika kuwa yeye anapaswa kukata leseni na kulipa kodi kama walivyo wafanyabiashara wakubwa.
Makamu wa Rais aliongeza kuwa kama shilingi 20,000/- zinaonekana ni nyingi kwa baadhi ya wafanyabiashara wadogo kulipa kwa mkupuo, uongozi wa Mkoa, Wilaya unaweza kuweka utaratibu ambao utawawezesha kulipa kwa awamu.
Alisema mfanyabiashara huyo anaweza kulipa kwa awamu mbili au tatu na akishamaliza malipo anakabidhiwa kitambulisho chake.
Aidha Makamu wa Rais alitoa angalizo kwa viongozi wa Mamlaka ya Mikoa na Serikali za Mitaa kuhakikisha hakuna Mfanyabiashara atakayepewa kitambulisho kabla ya kumaliza malipo yote kuwa upo uwezekano wa kutoroka na kwenda Mkoa mwingine na kuendesha shughuli zake kwa kutumia kitambulisho ambacho bado anadaiwa.
0 comments:
Post a Comment