Ni hali ambayo haijawahi kutokea Afrika na hata nje ya Afrika kwa mgombea urais kuamua kumchagua mama yake kuwa mgombea mwenza.
Hayo yametokea kwa mgombea urais wa Malawi, David Chirwa maarufu kama Ras Chikomeni aliyemteua mama yake, Niness Kayengo kuwa mgombea mwenza na pia amesema kwamba akichaguliwa atahalalisha bangi.
Mgombea urais urais huyo ambaye yeye ni mkulima mkubwa wa bangi anasema kwamba kitakachomsaidia kuingia kwenye urais ni kutetea zao la bangi akidai kwamba sera yake kubwa ni kuhalalisha zao hilo ili liheshimike na kuwa zao la biashara.
Chikomeni ambaye pia ni mwanamuziki maarufu ana miaka 41 na mama yake mzazi ana miaka 68.
Mgombea huyo ambaye wafuasi wake wengi ni vijana anawania urais Mei 21 mwaka huu ikiwa ni awamu ya nne tangu nchi hiyo kupata uhuru.
Awali hakupata wadhamini wa kutosha ndio maana fomu zake zikawa hazina vigezo kumpitisha kuwa mgombea urais wa Malawi lakini kwa sasa ametimiza vigezo vya kuwania urais wa nchi hiyo.
Alisema lengo la kumchagua mama mzazi kuwa mgombea mwenzake ni kwa sababu alikuwa mshauri wake wa karibu wa maisha yake yote.
“Mama yangu ni mshauri wangu wa karibu na maisha yangu yote anataka nifanikiwe kwenye maisha yangu na kuwa kiongozi wa nchi na pia ameshastaafu muda mrefu,’’ alisema
Alisema ana uhakika atakutana na changamoto nyingi sana wakati wa kampeni lakini hana budi kuzikabili kama mwanasiasa.
“Bila kukutana na changamoto hatuwezi kufanikiwa hasa sisi wanasiasa wachanga ambao ndio kwanza tunaanza kujiingiza kwenye siasa,’’ alisema.
Chanzo - Mwananchi
0 comments:
Post a Comment