KAMBI Rasmi ya Upinzani Bungeni, imelitaka Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuwafutia posho wabunge wa CCM
wanaofika kwenye vikao vya Bunge hilo na kukaa kimya bila kuchangia
jambo lolote hata kwa maandishi kwa maelezo kuwa hawafanyi kazi.
Msemaji
Mkuu wa Kambi hiyo, ambaye ni Mbunge wa Momba, David Silinde (Chadema),
alitoa pendekezo hilo jana bungeni mjini hapa muda mfupi kabla ya
kuwasilisha maoni ya Kambi ya Rasmi ya Upinzani Bungeni, kuhusu hotuba
ya Mapendekezo ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali katika
mwaka wa Fedha 2016/17.
Hotuba hiyo ya Bajeti iliwasilishwa bungeni Juni 8, mwaka huu na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango. Silinde alisema;
“Kabla
ya kutoa maoni ya Kambi ya Upinzani, ninaomba niweke sawa taarifa
zinazopotoshwa na kiti cha Naibu Spika kuhusu posho na kueleza kuwa sisi
ndio kila wakati tumetaka posho ziondolewe na kupelekwa kwenye shughuli
za maendeleo, lakini Serikali imekuwa ikisuasua kutekeleza jambo hilo.”
Kwa
mujibu wa Silinde, suala kwao sio posho kwa sababu hata wakati wa Bunge
la Katiba kila Mbunge wa upinzani aliacha Sh milioni 30.
Akizungumzia
wabunge wa CCM wakaa kimya, Silinde alisema wapo na wanapokea posho
kama kawaida ilhali hakuna kazi yoyote wanayoifanya na kwamba umefika
wakati sasa Bunge liongeze umakini zaidi kwa kuwadhibiti wabunge wa aina
hiyo kwa kuwakata posho za vikao.
Alipendekeza kuwa Hansard (kitabu cha taarifa rasmi za Bunge) zitumike kuwabaini kwa sababu wapo na wanajulikana.
Hata
hivyo, kabla ya kueleza suala hili, Silinde alivunja utaratibu kwa
kumtaja Naibu Spika kwa jina ‘Kiti cha Spika’ badala ya Mheshimiwa Naibu
Spika, jambo lililosababisha alazimishwe kutumia busara kuheshimu kiti
hicho na hatimaye kutii.
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana,Ajira na Wenye
Ulemavu), Jenister Mhagama, ndiye aliyesimama kuomba mtoa hoja
(Silinde), aheshimu utaratibu wa Bunge hilo.
0 comments:
Post a Comment