SERIKALI imesema shule zote zenye nafasi za wanafunzi wa kujiunga na kidato cha tano mwaka huu, zimejaa hivyo hakuna nafasi ya mwanafunzi kubadilishiwa shule au mchepuo aliochagua.
Hayo yalibanishwa jana katika taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya
habari mjini hapa na Msemaji wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (Tamisemi), Rebecca Kwandu.
Kwandu alisema baada
ya serikali kutangaza wanafunzi waliojiunga na kidato cha tano, baadhi
ya wazazi na wanafunzi wamekuwa wakifika ofisi za Tamisemi kuomba
kubadilishiwa shule au tahasusi (michepuo) walizochaguliwa.
“Tunapenda
kuwaarifu kwamba shule zote zenye nafasi za wanafunzi wa kujiunga na
kidato cha tano mwaka 2016 zimejaza, hivyo hakuna kinachoweza
kubadilishwa,” alisema Kwandu.
Aidha, Kwandu alisema vigezo
ambavyo vilitumika katika uchaguzi huo ni pamoja na ufaulu na uchaguzi
wa wanafunzi wenyewe juu ya masomo wanayopenda kuendelea nayo kidato cha
tano na sita.
“Kulingana na utaratibu uliowekwa na serikali,
mwanafunzi mwenye sifa za kuchaguliwa kuendelea kidato cha tano na vyuo
vya ufundi ni yule ambaye ufaulu wake ni kuanzia daraja la kwanza hadi
la tatu. Wanafunzi hao wamepangwa kulingana na ufaulu wao masomo
waliyochagua na nafasi zilizopo,” alisisitiza.
Pia alisema nafasi
za shule walizopangiwa wanafunzi zimezingatia miundombinu ya shule
husika na uwezo, na kwamba kila shule imepewa wanafunzi kulingana na
nafasi zilizopo, hivyo hakutakuwa na nafasi ya kuwabadilisha kutoka
shule moja kwenda nyingine kwa sasa.
Kutokana na hali hiyo,
aliwataka wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano na
vyuo vya ufundi kuripoti katika shule na vyuo walivyopangiwa kama
walivyoelekezwa.
Alisema mwanafunzi ambaye hataripoti ifikapo
Julai 24, ambayo ni tarehe ya mwisho kwa muda uliopangwa, atakuwa
amepoteza nafasi yake kwa kuwa itachukuliwa na mwanafunzi mwingine
ambaye hakupata nafasi awali.
0 comments:
Post a Comment