SERIKALI imesitisha ajira zote, kama njia ya kukabiliana na wimbi la watumishi hewa.
Kutokana na uamuzi huo hivi sasa hakuna nyongeza ya mishahara kwa
watumishi wa Serikali na wakala zake pamoja na utoaji wa vibali wa
likizo ya bila malipo.
Akizungumza na MTANZANIA jana jijini Dar es Salaam Katibu Mkuu
Utumishi, Dk. Laurean Ndumbaro, alisema kuwa Serikali imesitisha kwa
muda utoaji wa ajira, ili kupitia upya muundo wa Serikali na taasisi
zake.
Alisema utekelezaji wa mkakati huo utakwenda sambamba na kusitisha
kwa muda utoaji wa vibali vya ajira zote mbadala pamoja na uidhinishaji
wa ajira hizo zilizopo Sekreterieti ya Ajira katika utumishi wa umma na
kwenye mfumo wa taarifa za kiutumishi.
“Ni kweli tumesitisha kwa muda ili kupitia mfumo wa Serikali na hata
kuangalia ulipaji wa mishahara kama upo katika malipo stahiki.
“…na hili litakwenda sambamba na hata kusitishwa malipo ya mishahara
yanayotokana na upandishwaji wa vyeo kwa watumishi. Tukimaliza zoezi
hili ndipo tunaweza kuanza kutoa ajira za Serikali,” alisema Dk.
Ndumbaro.
Alisema muundo mpya wa utumishi wa Serikali unakwenda sambamba na
uhakiki wa malipo ya mishahara, hivyo ni lazima ujue ni nani unayemlipa
kuliko ilivyo sasa.
Kwa mujibu wa maelekezo hayo uhamisho na uidhinishaji katika mfumo wa
watumishi ambao wamehamishwa kutoka kwa mwajiri mmoja kwenda kwa
mwajiri mwingine ambao atalipwa mshahara mkubwa kuliko ule wa sasa pia
utaangaliwa kwa lengo la kupata taarifa sahihi za mtumishi husika.
“Baada ya kukamilika kwa zoezi la uhakiki watumishi pamoja na
tathmini ya muundo wa Serikali na taasisi zake, wote wataarifiwa ni lini
utekelezaji utaendelea,” alisema.
Taarifa kutoka maeneo mbalimbali nchini, zililiambia gazeti hili kuwa
maelekezo hayo yalitolewa Juni 13, mwaka huu na kusambazwa katika
maeneo mbalimbali ikiwemo kwa makatibu wakuu wote, makatibu tawala wa
mikoa, kwa wakuu wa idara za Serikali zinazojitegemea.
Waliotakiwa kutekeleza maelekeo hayo ya Serikali ni wakurugenzi wote
wa majiji, manispaa na miji, wakurugenzi watendaji wa halmashauri za
wilaya, watendaji wa taasisi za umma na watendaji wa wakala za Serikali
kwa upande wa Tanzania Bara.
Kamatakamata
Wiki iliyopita vyombo vya dola vilianza kuwatia mbaroni watumishi hewa kwa kuwafuata na pingu majumbani.
Hatua hiyo imetajwa kuwa ni mkakati wa Serikali ya awamu ya tano
chini ya Rais Dk. John Magufuli, kuanza kupambana na watendaji ambao
wamekuwa wakiisababishia hasara Serikali ya kulipa mamilioni ya shilingi
kwa watumishi hewa.
Kutokana na uamuzi huo ambapo mtumishi mmoja wa moja za za Mkoa wa
Kigoma, alifuatwa na askari wa polisi na kutiwa mbaroni nyumbani kwao
Ubungo Kibangu jijini Dar e Salaam.
Tukio hilo la aina yake lilitokea mchana wa juzi na kuibua hisia
miongoni mwa majirani ambao waliliambia gazeti hili kuwa, askari hao
walifika nyumbani kwao na mtumishi huyo na kumfunga pingu mikono na
miguuni na kuondoka naye.
Kutokana na hekaheka hiyo ya watumishi hewa, taarifa kutoka wilayani
Nyasa mkoani Ruvuma, zililieleza gazeti hili kuwa walimu watano wastaafu
nao walikamatwa na polisi kwa madai ya kupokea mishara hewa.
Mbali na walimu hao pia alikuwepo muuguzi mmoja.
Akizungumzia na MTANZANIA kuhusu tukio hilo la kamatakamata mmoja wa
waliokumbwa na hali hiyo, Marco Nyimbi ambaye ni mwalimu mstaafu wa
Shule ya Msingi Muungano wilayani Nyasa mkoani Ruvuma alisema hatua ya
kukamatwa kwake ilimfanya apigwe na butwaa na kushangazwa na hatua ya
kukamatwa yeye na wenzake watano kwa kudaiwa kuwa ni watumishi hewa.
Hivi karibuni akizungumza Dar es Salaam, Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki,
alisema Serikali imewaondoa jumla ya watumishi 12,246 kwenye mfumo wa
malipo ya mishahara kwa sababu mbalimbali, ikiwemo umri wa kustaafu kwa
lazima, kufukuzwa kazi, vifo na kumalizika kwa mikataba.
Waziri Kairuki alisema kuondolewa kwa watumishi hao kumeokoa Sh bilioni 25 ambazo zingelipwa kwa watumishi hao.
Alisema kuwa fedha hizo zingepotea endapo watumishi wasingeondolewa
kwenye mfumo, ikilinganishwa na watumishi 10, 295 walioondolewa kwenye
mfumo kuanzia Machi 15 hadi Aprili 30 mwaka huu.
Alisema pia kuwa watumishi hewa 1,951 wameongezeka ikiwa ni pamoja na Sh bilioni 1.8.
Alifafanua kuwa ofisi hiyo ilitoa maelekezo kwa Makatibu Wakuu, Wakuu
wa taasisi za umma na Mamlaka za Serikali za Mitaa, kuwasilisha taarifa
ya watumishi hewa ifikapo Juni 10, mwaka huu
chanzo: Mtanzania
0 comments:
Post a Comment