Aliyekuwa mgombea urais wa
Chadema, Edward Lowassa amesema hakuridhika na matokeo ya uchaguzi wa
Oktoba 25, na kwa kulijua hilo, ‘watawala’ walimleta rafiki yake kutoka
Nigeria, TB Joshua ili amshawishi akubali matokeo.
Lowassa alisema baada
ya TB Joshua, muhubiri na kiongozi wa Synagogie Church of All Nations,
kukaa naye pamoja na viongozi wengine wa Chadema na kumueleza jinsi
‘walivyoporwa’ ushindi, kiongozi huyo wa kidini alichukia na kusitisha
azma yake ya kuhudhuria sherehe za kumuapisha Rais John Magufuli.
TB
Joshua aliwasili nchini Novemba 3, siku mbili kabla ya kuapishwa kwa
Magufuli kuwa Rais, na alienda Ikulu na baadaye nyumbani kwa Lowassa
ambaye alitumia muda mwingi wa ziara yake pamoja naye.
“Walimuita rafiki
yangu TB Joshua, wakaenda wakampokea. Alipokelewa na Rais Magufuli,
akapelekwa Ikulu akazungumza na Kikwete,” alisema Lowassa.
“Baadaye
akawaambia wamlete kwangu. Kweli akaja nyumbani kwangu, tukazungumza
naye. Sitaki kusema mengi sana niliyomwambia, lakini moja, nilimwambia
ukikubali yale matokeo ndugu yangu, heshima yako itashuka hapa nchini na
duniani kwa ujumla,” alisema.
Lowassa alisema hayo jana alipokuwa
akizungumza katika mahafali ya Shirikisho la Wanafunzi wa Vyuo Vikuu
Wafuasi wa Chadema (Chaso) katika Ukumbi wa Karimjee jijini Dar es
Salaam.
Alisema ni kutokana na msimamo na mazungumzo waliyofanya na TB
Joshua ndio yaliyosababisha kiongozi huyo wa kidini maarufu barani
Afrika kutohudhuria sherehe hizo za kuapishwa zilizofanyika Uwanja wa
Taifa jijini Dar es Salaam.
Katika hotuba yake, Lowassa alimpongeza Rais Magufuli kwa jitihada
anazozichukua za kujaribu kufufua uchumi wa nchi, lakini akasema
hakubaliani na mbinu anazotumia.
Alisema anafurahia kumsikia Rais
Magufuli akiihubiri nchi ya viwanda, lakini hana imani na lugha
anazotumia.
“Rafiki zangu nawasikia na nafurahi sana wanasema wanataka
kujenga nchi ya viwanda. Natamani nchi hiyo, lakini lugha hiyo sina
imani nayo sana,” alisema.
Alisema haziamini lugha hizo kwa kuwa ni vitu
visivyowezekana kutokana na ukweli kuwa viwanda vilivyopo haviwezi
kufufuka na kuondoa tatizo la ajira lililopo nchini.
“Wanasema watafufua
viwanda,
lakini viwanda vilivyopo vili kuwa analojia sasa hivi mambo yote ni ‘digital’. Hicho
kiwanda kitafufuliwaje maana hata madukani spea zake hazipo labda
zitengenezwe upya,” alisema.
Alisema tatizo lililopo kwa sasa nchini ni
la ajira na kwamba hata kaulimbiu yao kwenye kampeni ilikuwa ajira kwa
kutambua kuwa wapo vijana wengi waliomaliza vyuo, hawana ajira na kwamba
eneo kubwa litakaloweza kuwaajiri ni sekta ya kilimo.
Lowassa, ambaye
pia ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chadema, alisema anakubaliana na
kauli iliyotolewa na Jenerali Ulimwengu aliyoitoa hivi karibuni kuwa
Rais Magufuli ameturudisha nyuma miaka 50, akiponda uamuzi wa Serikali
kuzuia matangazo ya Bunge kurushwa moja kwa moja.
“Uamuzi ule si mzuri
na una matatizo makubwa kwa kuwa ni kuwanyima wananchi haki yao muhimu
ya kuwasikiliza wawakilishi wao,” alisema.
Akizungumzia elimu, Lowassa
alisema wakati Chadema na Ukawa waliposema watatoa elimu bure kuanzia
chekechea mpaka chuo kikuu walikuwa wamejipanga, lakini Serikali imebeba
sera hiyo bila kujiandaa.
Aliwapongeza vijana kwa kuwa kiini cha
mabadiliko na kusema mpaka sasa akikutana na watoto wadogo wanamsalimia
kwa kumwambia “Mabadiliko Lowassa”.
Alisema vijana walifanya kampeni
nzuri na kumwezesha kupata kura nyingi zilizowapa ushindi, lakini
wakanyimwa ushindi.
“Tulishinda vizuri sana lakini hata hizo walizotupa,
zinatosha kuwaambia kuwa tuliwapa kazi ya kutosha. Nyie mnajua, wao
wanajua na mimi najua,” alisema.
Lubuva aondolewe
Alisema licha ya kumuheshimu mwenyekiti wa NEC, Jaji
Damian Lubuva, anapaswa kutimuliwa kwa kushindwa kuisimamia vyema tume
hiyo.
“Tume ya Uchaguzi inapaswa iondoke. It must go na ndio maana
nasema iko haja ya kuanza upya kudai Katiba mpya haraka iwezekanavyo,”
alisema Lowassa.
“Kama yupo mtu yeyote anayechukia matokeo ya uchaguzi
uliopita, suluhisho lake ni kuwa na tume huru ya Uchaguzi itakayotokana
na Katiba mpya. Tusipohangaika na Katiba mpya tutarudi palepale.”
Alirudia kauli yake kuwa baada ya uchaguzi kulikuwa na waliomtaka
atangaze “kuingia barabarani”, lakini aliwakatalia.
“Tutakuwa tunakwenda
Ikulu kwa kufagia barabarani kwa damu za watu. No, tutakwenda Ikulu
bila damu za watu wakati wowote na Mungu atatusaidia. Nawaambia wale
wote ambao hawakuridhika, mnajua nguvu ya umma lakini msiitumie
kuwaumiza watu,” alisema.
Aliwataka viongozi wote wa Chadema kujali
maslahi ya wanyonge kwa kuepuka kufanya kazi kwa mazoea.
Meya wa Jiji la
Dar es Salaam ambaye ni diwani wa Chadema, Charles Mwita aliwataka
wanafunzi kufanya kazi ya kukijenga chama kwani mabadiliko ya kweli
yataletwa na vijana.
Muasisi wa Chaso, Pamela Maasaio aliwataka vijana
wa Chadema kuachana na siasa za kwenye mitandao na badala yake waende
mitaani kupiga kelele na kuweka mikakati ya pamoja.
0 comments:
Post a Comment