WAKATI Naftal Mlawa ‘Nuh
Mziwanda’ anaanza safari yake ya muziki miaka kadhaa iliyopita, wengi
wetu tulikuwa hatuamini kama ipo siku anaweza kufikia hatua ya kufanya
muziki mzuri na kuweza kukubalika.
Wengi waliamini atasikika ndani ya muda
mfupi, atapotea kama ambavyo wengi wameibuka na kupotea kabla ya kufikia
hatua ya kupata umaarufu.
Hata alipojaribu kutupa karata yake kuwa
na uhusiano wa kimapenzi na mwigizaji Zuwena Mohammed ‘Shilole’, bado
watu walikuwa hawaelewi anafanya nini mjini.
Wengi waliamini hata suala la mapenzi ni
kiki tu za mjini. Hata alipokuja kuachwa, wengi waliamini pale ndiyo
ulikuwa mwisho wa safari yake.
Lakini waswahili wanasema Mungu hamtupi
mja wake, licha ya kuachwa kwa vitimbi na Shilole, kusakamwa mitandaoni
kuwa alikuwa akitembea na mtu aliyemzidi umri, hatimaye amefanikiwa
kufanya wimbo mkali wa Jike Shupa akimshirikisha fundi Alikiba Saleh
‘King Kiba’ ambao kwa sasa ni habari ya mjini.
Wimbo huo umekubalika. Unachezeka na video yake ni kali.
Je, Nuh anazungumziaje suala la
kuonekana amemuimba Shilole? Kwa nini aliamua kuimba wimbo huo? Idea
ilitoka wapi? Hapa chini pana mambo mengi zaidi:
Kwanza tuambie jina la wimbo wa Jike Shupa umelitoa wapi?
Hilo neno Jike Shupa amelitoa Alikiba wakati anaandika chorus yake.”
Unataka kutuambia haukuwa wimbo wako hadi jina alitoe Alikiba?
Hapana ni wimbo ambao nilikwishaurekodi
na chorus yangu nilikuwa nimeifanya nikawa nataka niuachie, lakini
nilipotafakari nikaona sijashirikiana na mtu, mashabiki wangu
hawajanizoea kwenye kolabo sasa hivi ngoja nirudi kitofauti.
Nikaona bora nimtafute Alikiba,
nikamsikilizisha wimbo, akaniambia mbona Nuh huu wimbo umeshaisha
halafu hapa ulivyoimba wewe mbona wimbo mkali, nikamwambia bro’mimi
nahitaji sauti yako. Naomba unisaidie.
Kiba ana jina kubwa, hakukuringia wakati unamuomba kolabo?
“Nashukuru Mungu hakuchomoa. Akaniambia
poa tutaenda studio, baada ya muda kama wiki mbili, tukaenda studio
tukarekodi wakatoa chorus yangu ambayo mimi nilisharekodi, Ali akanza
kuandika chorus yake ambayo ndiyo ikapatikana Jike Shupa ndani ya hiyo
chorus.
Sasa hii Jike Shupa ina maana gani? Imetokana na nini?
“Jike Shupa ni kitu ambacho pia
kilitukumbusha zamani mimi na Ali, sababu tulikuwa ni family friend.
Tunachezacheza wote zamani tukienda kwenye vigodoro, kuna wale wanawake
ambao hawajatulia tulikuwa tunawaita majike shupa tukiendaenda kwenye
vigodoro, kwa hiyo vitu kama hivyo tukaona poa tulitumie kwa sababu
tunalijua na ndiyo tumekua nalo, kwa hiyo kwa kifupi Alikiba ndiye
alitoa idea ya Jike Shupa. Namshukuru kwa kufanya kitu kikubwa kwangu.
Watu wanasema umemuimba Shilole baada ya kukutenda huko nyuma, unalizungumziaje hilo?
“Just idea tu, japo watu wengine
wanasema nimemuimbia mtu, lakini mimi niliimba kwa ajili ya jamii na
mashabiki wangu na watu ambao wametuzunguka sababu kama mapenzi si mimi
tu nimeumizwa, wapo wengi tu ambao wameumizwa. Sikujiangalia mimi tu
lakini niliangalia na mashabiki wangu.
Kati ya warembo waliowahi kukuumiza penzini ni Shilole, hukuhisi kwamba atajisikia vibaya pindi atakaposikiliza wimbo huu?
Muziki ni filings. Kuimba kile kitu
ambacho umekipitia. Haijalishi mapenzi na maisha magumu uliyopitia. Mimi
nanukuu marehemu Remmy Ongala, alipoimba Kifo alifiwa na mtu wake wa
karibu.
Kwa hiyo hivyo ni vitu ambavyo unaimba
kwa fillings. So hata mimi nimeimba kitu ambacho kimenitokea. Siwezi
kuimba tu kila siku vitu ambavyo vimewatokea watu wengine. Nafikiri ni
jambo zuri kuwapa hisia zangu ambazo naamini hata wao ‘wamezifili’.
Sasa unafikiri Shilole anafurahia kile ulichokifanya katika video kuigiza matendo yote mliyoishi naye?
Kama yeye imemuumiza, I don’t care. Mimi sijali kwa sababu mimi nimewapa hisia mashabiki wangu.
DONDOO:
Jina kamili: Naftal Mlawa
Umri: 24
Ngoma zake zilizobamba: Otea Nani, Zima Taa, Msondo Ngoma, Bilima, Ganda la Ndizi na Hadithi.
0 comments:
Post a Comment