MASHABIKI wa Yanga leo watajazana Uwanja wa Taifa,
Dar es Salaam bila kulipa hata senti tano kushuhudia mechi ya Kombe la
Shirikisho Afrika dhidi ya TP Mazembe kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Kongo (DRC).
Hata
hivyo, kujazana kwao uwanjani hakutakuwa na maana iwapo kikosi hicho
cha Kocha Hans van der Pluijm kitashindwa kuondoka na pointi tatu.
Katika mchezo wa kwanza wa mashindano hayo dhidi ya Mo Bejaia ya
Algeria, Yanga ililala kwa bao 1-0, hivyo mechi ya leo kuwa na kila
sababu ya kushinda hasa kwa kuzingatia itakuwa mbele ya mashabiki wake
wengi.
Awali, kulikuwa na mvutano kati ya Yanga na Shirikisho la Soka
Tanzania (TFF) baada ya klabu hiyo ya Jangwani kutangaza kuwa mashabiki
wataingia bure.
Hata hivyo, makubaliano ya mwisho yaliyolishirikisha pia Shirikisho
la Soka Afrika (Caf), mashabiki wasiozidi 40,000 ndiyo watakaoruhusiwa
kuingia uwanjani kutokana na sababu za kiusalama, kwa mujibu Msemaji wa
TFF, Alfred Lucas.
Lucas alisema kamisaa wa mchezo huo kutoka Zambia, Kidio Joseph
alikuwa na shaka huenda uwanjani ungejaa kupia uwezo, hivyo kuhatarisha
usalama.
"Hayo ni maelekezo tuliyoyapata kutoka CAF na Yanga wanazo taarifa hizi na ni lazima tufuate maelekezo hayo," alisema Lucas.
Aidha, alisema mashabiki wataruhusiwa kukaa kwenye jukwaa la mzunguko na majukwaa mengine watakaa watu maalum (Special Seat).
Aidha, kwa upande wa Yanga wamekubali maelekezo hayo ya CAF.
Afisa habari wa timu, Jerry Muro, alisema wamepata taarifa hiyo ya CAF na hawana pingamizi nayo.
Achana na habari hiyo, turudi kwenye mchezo wa Yanga na Mazembe.
Achana na habari hiyo, turudi kwenye mchezo wa Yanga na Mazembe.
Wawakilishi hao wa Tanzania, wataingia uwanjani wakiwa na dhamira
moja tu ya ushindi, kwani hata matokeo ya sare dhidi ya timu hiyo ngumu
hatawasaidia kujiweka kwenye nafasi nzuri.
Pluijm alisema wachezaji wake wanafahamu umuhimu wa ushindi kwenye
mchezo huo, kinyume na ushindi basi vijana hao wa Jangwani watakuwa
wamepotea njia.
"Kupoteza mchezo wa kesho (leo) itakuwa mbaya zaidi kwetu, kundi letu
lina timu nne na kati ya hizo mbili zilipata ushindi kwenye mechi zao
za kwanza," alisema Pluijm.
Pluijm, ambaye kikosi chake kiliweka kambi zaidi ya wiki mbili nchini
Uturuki kujiandaa na michuano hiyo, ana matumaini wakubwa wachezaji
wake watafuata maelekezo yake na kushinda mechi hiyo.
"Wachezaji wangu wako kwenye hali nzuri, wamejiandaa kikamilifu kwa
mchezo huu. Ukimuondoka Msuva (Simon), wengine wako kwenye hali nzuri
kimchezo," alisema na kuongeza:
"Tunahitaji kushinda leo mbele ya mashabiki wetu waliopata fursa ya
kuingia uwanjani bila kulipa kiingilio. Haitakuwa na maana kupoteza
mchezo huu, siyo tu kwa sababu mashabiki wetu wataingia uwanjani bura,
bali matokeo ya kipigo yatatuweka kwenye wakati mgumu."
TP Mazembe wanashuka dimbani wakiwa na kumbukumbu ya ushindi baada ya
kushinda mchezo wa kwanza, hivyo wamejipanga kikamilifu kuifunga Yanga
nyumbani
Katikati ya wiki hii, mshambuliaji Mazembe, Thomas Ulimwengu alisema
mchezo utakuwa mgumu kutokana na ukweli kwamba Yanga ni timu nzuri na
hawatakubali kupoteza mchezo mwingine baada ya kushindwa kupata pointi
kwenye mchezo wa kwanza.
"Tumejiandaa vizuri na mchezo huu, pamoja ya kuwa mpira una matokeo
matatu lakini kwetu tunaamini kwenye ushindi," alisema Ulimwengu.
0 comments:
Post a Comment