Saturday, 25 June 2016

Fanya haya ili usiishie kuzalishwa, kuachwa!

...

Couple sitting on sofa with arms folded, looking angry
KWA neema na rehema zake Mungu, mimi na wewe tunaendelea kukutana katika safu hii. Jumamosi nyingine ambayo ninaamini nimefumbata jambo kichwani ambalo lina faida. Chukua muda wako, soma na utafakari kwa makini kisha chukua hatua.
Kama mada inavyojieleza hapo juu. Matarajio ya wengi ni kuishi katika penzi salama. Kuishi na mwanaume au mwanamke wa ndoto yake. Lakini bahati mbaya sana, tofauti na matarajio, wengi hujikuta wakianguka katika mikono ambayo si salama.
Wanaishi katika penzi kipofu. Wanajisahau wakiwa penzini na kujikuta baadaye wakijuta. Mtu anawekeza nguvu nyingi kwa mtu ambaye si sahihi. Bahati mbaya sana nguvu ya penzi humfanya mtu awe kipofu. Anaweza kuona kabisa anaangamia lakini hashtuki.
Anauona moto mbele yake lakini anafikiri ni barafu. Matokeo yake anajikuta matatizoni. Wengi sana wamelia baada ya kujikuta wamedumu penzini na matapeli wa mapenzi. Mwanamke amepewa matumaini, ahadi kemkemu kwamba ataolewa lakini kumbe mwanaume ni tapeli.
Anapewa matumaini kwamba ataolewa. Uongo unamuingia kwelikweli. Anaruhusu kubeba mimba ya kwanza, anajifungua. Anabeba mimba nyingine, anajikuta amezaa mtoto wa pili. Mwanaume anaendelea kumpa moyo na matokeo yake hata mtoto wa tatu, mwanaume anaanza visa na baadaye kuingia mitini.
Hapo ndipo mwanamke anatamani kujiua. Anawaona wanaume wote duniani ni maadui. Anajuta kupoteza muda. Analia kwa mengi. Kwanza anaumia kudanganywa na mtu ambaye yeye alimpenda. Anaumia kwa sababu tayari ujana unakuwa umemtupa mkono.
Anajuta kwamba pengine angegundua mapema madhumuni ya mwanaume huyo, angeiahirisha safari mapema. Kwa kuwa umri tayari unakuwa umemtupa mkono, ‘soko’ lake pia linakuwa limepungua. Uwezekano wa kutokea mwanaume mwingine ili aweze kumuoa unakuwa mdogo.
Anaumia kila anapowaangalia wale watoto ambao wote wanahitaji mahitaji kutoka kwake. Ataumia zaidi pale mwanaume huyo anapooa mwanamke mwingine bila kujali kwamba amempotezea muda.
Bahati mbaya sana mateso hayo huwa yanakuwa upande wake. Mwenzake anafurahia maisha mapya ya ndoa na mwanamke mwingine. Akiwa mstaarabu atampa mahitaji, asipokuwa mstaarabu hatatoa mahitaji kwa watoto.
Ameziba milango kwa mwanamke wake wa awali, yeye milango inazidi kufunguka kwa kupata mwanamke mwingine. Tatizo hilo laweza kumtokea pia mwanaume lakini wachambuzi wengi wa masuala ya uhusiano wanasema lina madhara zaidi kwa wanawake.
Mwanaume anaweza kuingia kwenye ndoa akiwa na miaka zaidi ya hamsini lakini kwa mwanamke ni nadra. Mwanamke taa nyekundu inawahi zaidi kumuwakia kulingana na maumbile.
NINI CHA KUFANYA?
Unapaswa kutathmini mwenendo wako kila wakati. Usikubali kuishi na mtu ambaye kuna mahali unamtilia shaka. Ukiwa katika hatua ya awali, jiulize mtu uliye naye ni sahihi kwako? Ana sifa za kuwa baba wa watoto wako?
Ana sifa za kuwa mume? Anahitaji kweli kuishi kwenye maisha ya ndoa na wewe? Si mhuni? Maana wapo watu wana sifa za kuwa wahuni miaka yote. Anaishi maisha ya anasa. Yasiyofikiria kesho yake, asiyefikiria kwamba kuna wakati na yeye atatakiwa kuwa baba.
Kwake yeye ni kujirusha kwenda mbele. Kamwe hawezi kukupa wazo la kimaendeleo. Mtu wa aina hiyo muepuke mapema. Jiulize mtu uliye naye,  si mjanja mjanja? Historia ya maisha yake ipoje? Ana hofu ya Mungu?
Mungu ndiye aliyeweka mpango sahihi wa mwanaume kuwaacha wazazi wake na kwenda kuishi na mkewe, muombe yeye akupe mwenza sahihi wa maisha yako.
Mwenendo wa mtu hauwezi kujificha kwa miaka miwili mitatu. Atabainika tu. Usiruhusu ujauzito wakati mtu uliyenaye una shaka naye. Ikiwezekana mnaweza mkasubiri hadi pale mtakapoingia kwenye ndoa. Muombe Mungu akupe mtu ambaye atakuwa ni sahihi na asije kukutenda!
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger