JUNI 20, 2016
DODOMA
A.
UTANGULIZI
1.
Mheshimiwa
Spika, napenda kutumia fursa
hii kukushukuru wewe binafsi, Naibu
Spika na Wenyeviti wa Bunge kwa kuendesha vizuri majadiliano kuhusu Taarifa ya Hali
ya Uchumi wa Taifa 2015 na Mpango wa Maendeleo wa 2016/17 pamoja na Makadirio
ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka 2016/17, niliyowasilisha tarehe 8
Juni, 2016.
2.
Mheshimiwa
Spika, Kipekee, ninampongeza sana Mhe. Naibu Spika kwa
umahiri na weledi wa hali ya juu alioonesha katika kusimamia Kanuni za Bunge
wakati wote wa kikao hiki cha Bunge la bajeti. Hakika viwango vyake ni vya
kimataifa. Japokuwa Mhe. Joseph Kakunda, mwanafunzi wangu Idara ya Uchumi Chuo
Kikuu cha Dar-es-Salaam alichomekea sehemu fulani akidai kwamba mimi ni bahiri,
(nadhani alimaanisha bahiri wa kutoa maksi za upendeleo!), nataka niliambie Bunge lako tukufu kwamba kwa
viwango ambavyo Mhe. Naibu Spika alivyoonesha humu ndani, hakika ningempa maksi
za haki asilimia 100 kama walivyofanya maprofesa wake wa sheria UD na UCT.
Hongera sana.
3.
Mheshimiwa
Spika, napenda kutambua
michango iliyotolewa na: Kamati ya Bajeti, chini ya M/kiti wake Mheshimiwa Hawa
Abdulrahman Ghasia, Mbunge wa Mtwara Vijijini; Mheshimiwa David Ernest Silinde,
Mbunge wa Momba, Naibu Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu
Wizara ya Fedha na Mipango, na waheshimiwa Wabunge wote waliochangia kwa
kuzungumza au kwa maandishi hapa Bungeni. Ninawashukuru wote.
4.
Mheshimiwa
Spika, jumla ya Wabunge 158
wamechangia hoja niliyowasilisha. Kati ya hao, 133 wamechangia kwa kuzungumza
na 25 kwa maandishi.
B: HATUA ZILIZOPONGEZWA NA WABUNGE WENGI
5.
Mheshimiwa
Spika, Hatua zilizopongezwa na Wabunge wengi wakati wa mjadala juu ya Mpango wa
Maendeleo wa Taifa na Bajeti ya Serikali 2016/17 ni pamoja na zifuatazo:
·
Kuthubutu
kutenga asilimia 40 ya bajeti yote kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo,
ikiwa pamoja na kuanza ujenzi wa reli mpya ya kati kwa kiwango cha standard
gauge, barabara, umeme, ununuzi wa meli mpya ziwa Victoria na ndege tatu za
abiria;
·
Kuongeza
ukusanyaji wa kodi na mapato yasiyo ya kodi hadi kufikia wastani wa shilingi
1.2 trilioni kwa mwezi kwa kuziba mianya ya uvujaji wa mapato na kuimarisha
matumizi ya vifaa vya kielektroniki (EFDs) katika ukusanyaji wa mapato, na
Hazina kutoa fedha hizo kama ilivyopangwa;
·
Kusimamia
nidhamu ya matumizi na kupunguza matumizi yasiyo ya lazima ikiwa pamoja na
safari za nje, posho, sherehe, kuondoa watumishi hewa katika utumishi wa umma;
·
Kuhimiza
azma ya kufanya kazi na kurejesha nidhamu ya watumishi kazini kwa ajili ya
maendeleo ya Taifa;
·
Kuwapunguzia
wafanyakazi mzigo wa PAYE na SDL kwa waajiri;
·
Kuanzisha
mahakama ya kushughulikia mafisadi;
·
Kuweka
kipaumbele katika kufufua na kujenga viwanda ili kupanua fursa za ajira na wigo
wa kodi; na
·
Kujielekeza
kutekeleza Ilani ya CCM 2015, ahadi za viongozi wakuu na Dira ya Taifa ya
Maendeleo 2025 ili kutatua kero za wananchi, hasa masikini.
0 comments:
Post a Comment