Watu 9 kati ya 14 waliokuwa wameshikiliwa na polisi kwa tuhuma za
mauaji yaliyotokea katika msikiti wa Rahman, Mkolani jijini Mwanza
wameachiwa huru baada ya kuonekana hawana hatia.
Akizungumza na
nyumbani kwao mtaa wa Nyanghingi jana, mmoja wa watu hao, Hamidu Said
(31) alisema akiwa na wenzake tisa, waliachiwa Mei 30 baada ya kuonekana
hawahusiki katika tukio hilo.
Said alikamatwa Mei 18, muda mfupi baada ya kufika eneo la tukio kushuhudia mauaji hayo.
“Kati
ya watu tisa tulioachiwa, wanaume tulikuwa watano, wanawake wawili na
watoto wawili mmoja akiwa na miaka 13, mwingine 16,” alisema Said.
“Sikuamini kama natoka rumande, ila namshukuru Mungu kwa jinsi alivyonitetea hadi kuona sina hatia,” alisema.
Akizungumzia
tukio la mtoto wake kukamatwa, baba wa Hamidu, Said Bahebe, alisema ni
vigumu kuelezea mshtuko na machungu waliyoyapata baada ya kijana wao
kukamatwa na polisi, hivyo alilazimika kumuombea dua kwa kuachiwa baada
ya kukutwa hana hatia.
Alisema kama ambavyo hawakuamini siku
waliposikia kijana wao amekamatwa wakati ameenda kushuhudia tukio,
kadhalika hawakuamini kuona anaruhusiwa kurudi nyumbani.
“Hatukutegemea kama angetoka ndani mapema,” alisema.
Bahebe
alisema kwa siku 13 alizokaa rumande kijana wake, familia haikuwa na
amani na ilikosa raha wakidhani ataishia jela.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza,
Ahamed Msangi alisema wamewaachia watu hao ambao walionekana hawana
hatia, lakini bado wanafuatilia wengine ambao wanaonekana kuhusika na
tukio hilo bila ya kutaja idadi ya watu waliochiwa.
“Wapo baadhi
walioachiwa, wengine watafikishwa mahakamani wakati wowote baada ya
kuona ushahidi una kila aina ya dalili za kuhusika na tukio hilo,” alisema Msangi.
Katika
mauaji hayo, watu watatu waliuawa kwa kukatwa mapanga wakiswali
msikitini akiwamo Imamu wa Msikiti wa Rahman, Feruz Ismail (27), Mbwana
Rajab (40) na Khamisi Mponda (28).
Ilielezwa kuwa kabla ya
kuanza kuwashambulia waumini kwa mapanga, wavamizi hao waliamuru watoto
waliokuwamo msikitini humo kutoka nje kupitia mlango wa nyuma unaotumiwa
na wanawake.
Katika tukio hilo, mtoto Ismail Abeid (13)
alinusurika baada ya kupita kwenye mlango mwingine, tofauti na ule ambao
wavamizi walielekeza utumike ambako walijeruhiwa kwa kukatwa na mapanga
vichwani walipopita.
0 comments:
Post a Comment