Thursday, 10 January 2019

Utafiti : KUZAA OVYO CHANZO CHA UGONJWA WA MOYO

...
Utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Huazhong nchini China, umegundua kwamba kuzaa bila mpangilio husababisha maradhi ya moyo.

Unasema kila mwanamke anapojifungua, huwa ameingia katika hatari ya kupata ugonjwa wa moyo miaka michache baadaye.
Utafiti huo uliokuwa chini ya mtaalamu wa masuala ya afya, Dk. Dongming Wang, ulitokana na takwimu zilizokusanywa kutoka kwa wanawake zaidi ya milioni tatu.
Ugonjwa wa moyo unatajwa kuwa ni tishio nchini Uingereza, ambapo zaidi ya watu milioni saba nchini humo wanakabiliwa na ugonjwa huo.
Hali ni mbaya pia barani humu kwani utafiti wa mwaka 2016 uliwahi kueleza kuwa Afrika Kusini hupoteza takribani watu 210 kwa siku kutokana na ugonjwa huo.
Ripoti ya Dk. Wang na jopo la watafiti ilibainisha kuwa mwanamke aliyejifungua huwa na asilimia 14 ya kusumbuliwa na ugonjwa huo ambao kwa sasa unachangia asilimia 31 ya vifo vyote duniani.
Awali, miongoni mwa sababu kubwa zilizokuwa zikitajwa ni uvutaji sigara, kutozingatia mlo kamili, unene, matumizi ya pombe kupita kiasi na kutofanya mazoezi, ambapo husababisha ugonjwa huo kwa asilimia 50.
Wakielezea uhusiano uliopo kati ya kujifungua na ugonjwa huo, Dk. Wang na wenzake wanasema ni kwa kuwa moyo hutumia nguvu nyingi wakati wa ujauzito kuwahudumia mama na mtoto.
Wanasema kuna uwezekano wa asilimia tatu kwa mwanamke aliyejifungua kupata ugonjwa wa kiharusi miaka michache baadaye.
Ni kwa mazingira hayo, wataalamu wa afya wanawashauri kuwapa elimu kuhusu afya ya uzazi wanawake wenye ujauzito au waliojifungua ili kujinasua katika hatari hiyo.
“Madaktari wana kazi kubwa hapa. Wanawake wanatakiwa kutambua kuwa na watoto kunawaweka kwenye hatari ya kupata ugonjwa wa moyo au kupooza. Mimba za mara kwa mara ni hatari zaidi,” anasema Dk. Wang.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Ugonjwa wa Moyo ya Uingereza, Jeremy Pearson, anasema:
“Utafiti huo umethibitisha rasmi kuwa wanawake wenye watoto zaidi ya wawili wamejiweka hatarini zaidi.
“Huo ni ujumbe kwa wanawake, kwamba wanatakiwa kuwa makini ili kuitunza mioyo yao, ingawa huenda isiwe rahisi kwa kuwa wengi wanapenda kuwa na watoto.”
Akirejea majibu ya utafiti, Dk. Wang anasema wanawake wenye watoto wanatakiwa kuangaliwa kwa kuelimishwa namna wanavyoweza kuishi baada ya kujifungua, ikiwamo kuepuka mitindo ya maisha inayoweza kuitesa mioyo yao.
Licha ya kazi hiyo nzuri ya Chuo Kikuu cha Huazhong, zipo tafiti nyingi zilizoonesha umuhimu wa mwanamke kuzaa, ukiwamo ule uliofanywa Agosti, mwaka juzi na Taasisi ya Tafiti za Saratani ya Marekani (AICR).
Katika utafiti wao, walibaini kuwa mwanamke anayenyonyesha huwa na uwezekano mkubwa wa kuepuka saratani ya matiti katika siku za usoni. AICR ilionesha kuwa kwa miezi mitano tu ya mwanzo aliyonyonyesha, hujiweka mbali na ugonjwa huo kwa asilimia mbili.
Kama ilivyo kwa ugonjwa wa moyo kule Uingereza, wanawake wa Marekani wanasumbuliwa zaidi na saratani ya matiti, ambapo inaelezwa kuwa kati ya wanane, mmoja ana ugonjwa huo na maambukizi mapya yalifikia 266,000 kwa mwaka jana pekee.
Na Hassan Daudi na Mitandao
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger