Spika wa Bunge Job Ndugai, amesema kwa sasa Bunge limesitisha kufanya kazi na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad.
Kutokana na hali hiyo, amewatawanya wajumbe wa Kamati za Bunge za Hesabu za Serikali (PAC) na ile ya Hesabu za Serikali za Tawala za Mikoa na Mitaa (LAAC) kufanya kazi katika kamati nyingine.
Hatua ya usitishaji huo inatokana na kauli ya Profesa Assad aliyoitoa Desemba mwaka jana katika mahojiano na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa, Arnold Kayanda.
Mtangazaji huyo alimuuliza CAG kuwa ni vipi ofisi yake imekuwa ikijitahidi kila mwaka kufanya ukaguzi na kutoa ripoti zenye kuonesha kuna ubadhirifu, lakini baada ya hapo wananchi hawaoni kinachoendelea.
Katika majibu yake CAG alisema; “Hilo ni jambo ambalo kimsingi ni kazi ya Bunge. Kama tunatoa ripoti zinazoonyesha kuna ubadhirifu halafu hatua hazichukuliwi, huo kwangu ni udhaifu wa Bunge".
“Bunge linatakiwa kusimamia na kuhakikisha pale panapoonekana kuna matatizo basi hatua zinachukuliwa",Aliongeza Profesa Assad.
Spika Ndugai jana alisema suala hilo si la utani kama baadhi ya wanasiasa wanavyolichukulia.
Chanzo:Mpekuzi
0 comments:
Post a Comment