Saturday 31 August 2019

Waziri wa Ulinzi Dkt. Hussein Mwinyi aridhishwa na miradi ya SUMA JKT Kanda ya Ziwa

...
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi amesema anaridhishwa na kazi nzuri inayofanywa na miradi inayotekelezwa na SUMA JKT kanda ya Ziwa.

Dkt. Mwinyi akiwa kwenye ziara yake ya kukagua miradi inayotekelezwa na SUMA JKT pamoja na makampuni mengine yaliyo chini ya Wizara hiyo kanda ya Ziwa  tarehe 30/08/2019 katika Wilaya ya Kahama, Mkoa wa Shinyanga amesema kwa kiwango kikubwa ameridhishwa na kazi zinazofanywa na sehemu kubwa kazi zimekwenda kwa kiwango kinachotarajiwa na kuwa changamoto zilizopo zitafanyiwa kazi.

“Niwahakikishie Mikoa na Halmashauri zinazohusika na miradi inayotekelezwa na SUMA JKT changamoto zote zitafanyiwa kazi” amesema Dkt. Mwinyi.

Aidha, amemshukuru Mhe. Rais John Magufuli kwa kuiamini kampuni hiyo iliyo chini ya Wizara yake na ndiyo sababu ya yeye kufanya ziara hiyo ili kuhakikisha imani hiyo inadumu pamoja na kuwaomba viongozi wote wa Mikoa na Halmashauri kuendelea kuiamini.

Aidha, amewataka SUMA JKT kuongeza kazi ya ziada mara watakapopata fedha ili kukamilisha jengo la Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Msalala ambalo ujenzi wake umesimama kutokana na changamoto ya fedha.

Naye Mkurugenzi wa SUMA JKT Kanali Rajab Mabele amesema kuwa, kampuni hiyo imepiga hatua kubwa hasa katika nyanja ya ujenzi lakini pia inajihusisha na kazi nyingine mbalimbali ikiwemo kilimo na ufugaji.

Awali, akimkaribisha Dkt. Mwinyi Mkoani hapa, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack amemuomba kupitia kampuni ya SUMA JKT kuangalia jinsi ya kuwa na miradi ya kuvuna maji ili wananchi waweze kujishughulisha na kilimo cha umwagiliaji.

“Pamoja na kiangazi kilichopo, tunapata mvua nyingi sana na tunavuna mpunga unaoweza kulisha nchi yote, sasa tuone namna bora ya kuvuna hayo maji na tayari baadhi ya wananchi wameshaanza kuchimba mashimo makubwa ya kuvuna maji, tumeona kama Mkoa tufanye hilo ili wananchi wetu waweze kupata mpunga” amesema Telack.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger