Saturday 31 August 2019

KIJANA ASULUBIWA KAMA YESU KWA KUPIGILIWA MISUMARI KARIBU NA KITUO CHA POLISI

...

 Polisi nchini Uganda inachunguza kisa cha mwanamume mmoja aliyeshambuliwa kisha kupigiliwa misumari katika msalaba.

Inadaiwa mwanaume mwenye umri wa miaka 21 alishambuliwa na watu wawili wasiojulikana Alhamisi Agosti 29,2019 kwa madai ya kuunga mkono chama tawala cha National Resistance Movement (NRM) kinachoongozwa na Rais Yoweri Museveni.

Polisi nchini Uganda ilimtaja mwanaume huyo kuwa ni Baker Kasumba anayedaiwa kushambuliwa na watu hao alipokuwa akitoka kazini kuelekea nyumbani kwake eneo la Kalerwe.

Gazeti la Daily Monitor la Uganda limeripoti kuwa Kasumba alidaiwa alishikwa na kupigiliwa misumaru kwa nyundo na watu hao waliokuwa wamevaa kofia za chama cha NRM zinazovaliwa na wanachama wa chama hicho.

Kwa mujibu wa gazeti hilo, mwanaume huyo alipata usaidizi kutoka kwa wapitanjia waliomkuta akining’inia katika msalaba huo akiwa amewekewa kofia ya chama hicho katika mikono yake na kumpeleka katika Kituo cha polisi cha Kalerwewa kwa ajili ya kuripoti tukio hilo.

Inadaiwa kuwa mwanaume huyo aliokolewa na wanawake wawili walioshuhudia tukio hilo na kupiga mayowe hatua ambayo iliwafanya washukiwa kukimbia na kumuacha akining’inia.

Mwanaume huyo ambaye ni mfuasi wa chama cha NRM katika maelezo yake aliyoandika polisi alisema watu hao walimueleza kuwa wameamua kumsulubu ili afe kwa ajili ya chama anachokienzi.

Polisi wanadai kuwa kabla ya tukio hilo mwanaume alionywa na mfanyakazi mwenzake kutomuunga mkono Rais Museveni na chama chake.

Tukio hilo limeibua mjadala katika mitandao ya kijamii ambako wananchi wa Uganda wamelaani na kuonya siasa za chuki.

Kupitia mtandao wake wa Twitter, Judith Kukundakwe Asiimwe anadai kuwa hatua hiyo ni njama ya inayoendeshwa na kikosi maalum cha usalama kinachofahamika ili kuchafua sifa ya vijana wa chama cha upinzani.

Roxanne Daphne aliandika “hili ni kosa kubwa sana, sote tuna uhuru wa kuwa na maoni yetu ya kisiasa''aliandika.

Hata hivyo, Naibu msemaji wa polisi mjini Kampala, Luke Owoyesigyire alisema kuwa tayari polisi wameanza msako ili kubaini watu hao.

Tukio hilo la kushangaza kwa mujibu wa Daily Monitor lilitokea karibu mita 30 kutoka Kituo cha polisi cha Kibe na mpaka sasa mwanaume huyo anaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali kuu ya Mulago.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger