Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dkt. James Mataragio akipeana mkono na Mtendaji Mkuu wa Chiyoda Corporation Ndg. Ken Nagao baada ya kikao baina ya ujumbe wa Tanzania na Kampuni ya Chiyoda. Wengine pichani kutoka kushoto ni Ndg. Pius Gasper (TANESCO), Dkt. Tito Mwinuka, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Mhandisi Innocent Luoga, Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu (Wizara ya Nishati), Ndg. Katsuo Nagasaka (Chiyoda) na Ndg. Koji Nishita (Chiyoda).
Ujumbe wa Tanzania ukiwa katika kikao na Kampuni ya JGC kilichofanyika sambamba na kilele cha Mkutano wa Saba wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika (TICAD7). Upande wa kushoto ni Ndg. Kenji Yamamoto (JGC), Ndg. Masayuki Sato (JGC), Ndg. Yanamaka (JGC) na Ndg. Taketoshi Shogenji (JGC). Upande wa Kulia ni Mhandisi Innocent Luoga, Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu (Wizara ya Nishati), Dkt. James Mataragio, Mkurugenzi Mtendaji (TPDC) na Ndg. Pius Gasper (Tanesco).
***
Yokohama, Japan.
Kampuni kubwa za Japan zenye uzoefu wa miaka mingi katika miradi ya gesi asilia zimeonesha nia ya kuwekeza nchini Tanzania hususan katika mradi mkubwa wa kusindika gesi asilia (Liquefied Natural Gas-LNG). Kampuni za JGC na Chiyoda zenye uzoefu wa miaka mingi katika kazi za uhandisi, manunuzi na ukandarasi (EPC) hususan katika kutekeleza miradi ya LNG duniani zimekutana na ujumbe wa Tanzania uliohudhuria kilele cha Mkutano wa Saba wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika (TICAD7) zikionyesha nia ya kushiriki katika mradi wa ujenzi wa mitambo ya kusindika gesi asilia (LNG).
Katika kikao hicho kilichofanyika sambamba na TICAD7, Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC Dkt. James Mataragio alisema “katika kipindi cha muongo mmoja, Tanzania imepiga hatua kubwa katika sekta ya mafuta na gesi asilia ikiwa ni pamoja na ujenzi wa miundombinu mikubwa ya kusambaza gesi kwa ajili ya umeme, viwanda na majumbani”.
Dkt. Mataragio pia alieleza nia ya Serikali ya Tanzania kuwekeza katika utekelezaji wa mradi wa kimkakati unaokadiriwa kugharimu dola za marekani bilioni 30 na utahusisha uendelezaji wa kiasi kikubwa cha gesi asilia kilichogunduliwa katika kina kirefu cha bahari.
Dkt. Mataragio alieleza kwamba kwa sasa Serikali iko katika hatua za majadiliano ya vipengele muhimu vya mkataba wa Serikali mwenyeji (Host Government Agreemet-HGA) na kampuni za kimataifa zilizogundua gesi asilia katika kitalu namba 1, 2 na 4. Kitalu namba 1 na 4 vinaendeshwa na Kampuni ya Shell ikishirikiana na Ophir Energy na Pavilion wakati kitalu namba 2 kinaendeshwa na Kampuni ya Equinor ikishirikiana na ExxonMobil.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Chiyoda Corporation, Ndg. Ken Nagao alisema “Kwa miaka kadhaa sasa tumeshirikiana na Tanzania katika kuendeleza sekta ya gesi asilia na tunadhani tunaweza kushirikiana zaidi katika kutoa uzoefu tulionao wa zaidi ya miaka 50 katika ujenzi wa mitambo ya LNG”.
Kampuni ya Chiyoda imehusika katika ujenzi wa miradi mikubwa ya LNG ikiwemo Australia, Nigeria, Qatar na nchi nyingine nyingi ikiwa na pato ghafi la takribani Trilioni 7.2. Nae Mwenyekiti na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya JGC, Ndg. Masayuki Sato alieleza nia ya kampuni yake kushirikiana na Tanzania katika kuhakikisha Wananchi wake wanafaidika na rasilimali ya gesi asilia kwa kujenga mitambo ya LNG itakayowezesha uvunaji wa gesi asilia iliyogunduliwa katika kina kirefu cha bahari ya Hindi.
Akizungumza katika kikao hicho, Ndg. Sato alisema “Tumeshirikiana na Tanzania katika maandalizi ya mpango kabambe wa matumizi ya gesi asilia (NGUMP) na tusingependa kuishia hapo kwani tunadhani Tanzania ina fursa ya kuwa kituo kikubwa cha kuzalisha na kusambaza gesi asilia kwa nchi zenye mahitaji makubwa ya nishati na hivyo kukuza uchumi na pato la Taifa”.
JGC ni miongoni mwa kampuni kubwa katika ujenzi wa mitambo ya LNG na ujenzi wa miundombinu mingine katika mnyororo wa thamani wa gesi asilia, alifafanua zaidi Mwenyekiti na Mtendaji Mkuu wa JGC.
Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga nae alieleza nia ya Wizara ya Nishati kuhakikisha gesi asilia inatumika katika kukuza uchumi wa ndani kwa kuisambaza kwa viwanda vingi zaidi ili kuchochea ajenda ya uchumi wa viwanda itakayosaidia Tanzania kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
“Mpango kabambe wa matumizi ya gesi asilia unaainisha wazi kwamba tutatumia gesi yetu kusaidia kukuza uchumi na kunyanyua sekta nyingine kama vile viwanda, kilimo, uvuvi, usafirishaji na nyinginezo ili kubadilisha uchumi wa Taifa na watu wetu” alisema Mhandisi Luoga.
0 comments:
Post a Comment