Tuesday, 27 August 2019

Serikali Yatenga Milioni 696 kukarabati Shule kongwe ya Galanos iliyopo Tanga

...
Serikali imetoa zaidi ya shilingi milioni 696 kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya shule kongwe ya sekondari Galanos iliyopo mkoani Tanga.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknlolojia William Ole Nasha alipotembelea shule hiyo kukagua maendeleo ya ukarabati wa miundombinu ambapo amesema fedha hizo zimetolewa kupitia mradi wa Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R) katika mpango unaolenga kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia katika shule hiyo kongwe.

Ole Nasha amesema fedha hizo ni sehemu ya fedha zilizopelekwa katika shule kongwe nchini ambazo zinafanyiwa ukarabati mkubwa lengo likiwa ni kuzirudisha katika hadhi yake ya awali ili ziwe na mazingira mazuri yanayomwezesha mwanafunzi kujifunza na kufaulu vizuri

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri huyo amemtaka Mkurugenzi wa Jiji la Tanga, Daudi Mayeji kufuatilia kwa karibu sababu zilizopelekea kukiukwa kwa masharti ya mkataba wa muongozo wa ukadiriaji majenzi (BOQ) ambao ulielekeza kuwekwa chuma katika varanda za madarasa zinazoruhusu hewa na badala yake yamewekwa matofali ya kuchoma.

“Galanos tumeleta fedha zaidi ya shilingi milioni 696 kwa ajali ya kukarabati miundombinu, baada ya kukagua maendeleo ya ukarabati nimegundua kuna mapungufu makubwa ya kimakusudi, Mfano kwenye madarasa kulitakiwa kuwekwe chuma lakini badala ya kuweka chuma wameweka matofali ya kuchoma bila hata kufuata taratibu wa kufanya mabadiliko” amesema Ole Nasha.

Amesema inashangaza kwani Mhandisi alishiriki katika uandaaji wa BOQ hiyo na ni mmoja wa walioshauri kuwekwa kwa chuma lakini katika utekelezaji wa BOQ hiyo iliyopitishwa amebadili maelekezo, hata baada ya kamati ya ujenzi kumkatalia na kumtaka kufata BOQ inavyotaka lakini bado aliendelea na utaratibu wa kuweka matofali hayo badala ya chuma.

“Ndio maana nimemwelekeza Mkurugenzi wa Jiji afuatilie kwanini kuna ukiukwaji wa makusudi wa kuacha kufuata BOQ na nimemwelekeza achukue hatua kwa yeyote anayehusika kubadilisha maelekezo ya BOQ” amesisitiza Ole Nasha

Mkurugenzi wa Jiji la Tanga, Daudi Mayeji ameahidi kufatilia suala hilo la uwekwaji wa matofali badala ya chuma na kwamba atachukua hatua kwa wale wote waliohusika katika kubadili maelekezo yaliyopo katika mkataba wa ukadiriaji majenzi (BOQ).


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger