Tuesday 3 June 2014

MAZISHI YA MTOTO NASRA ALIEFICHWA KWENYE BOKSI KWA MIAKA 4

...



Mazishi  ya mtoto Nasra Rashid (4) aliyefichwa katika boksi tangu akiwa na umri wa miezi tisa, yanatarajiwa kufanyika leo katika makaburi ya Kola mkoani Morogoro.
 
Nasra alifariki dunia usiku wa kuamkia Juni mosi mwaka huu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alikokuwa akipatiwa matibabu kuanzia Mei 26 mwaka huu akitokea hospitali ya Morogoro.
 
Kwa mujibu wa Ofisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Morogoro, Oswin Ngungamtitu, ibada na heshima za mwisho zitafanyika katika Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
 
Alisema mwili wa Nasra utawasili katika Uwanja wa Jamhuri saa mbili asubuhi ambapo ibada na heshima za mwisho zitaanza muda huo hadi saa sita mchana.
 
Ngungamtitu alisema shughuli za mazishi zitaongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Said Amanji.
 
Mtoto Nasra alifariki usiku wa kuamkia Juni Mosi baada ya kuzidiwa kutokana na tatizo la kupumua na utapiamlo uliokuwa ukimsumbua alipofikishwa Muhimbili.
 
Safari kutoka Dar
Mwili wa Nasra jana uliondolewa katika hospitali ya Muhimbili majira ya mchana ukiwa ndani ya Toyota Noah iliyokuwa na askari polisi kitengo cha Upelelezi Mkoa wa Morogoro pamoja na watu wengine wawili ambao hawakujulikana nyadhifa zao.
 
Ofisa Uhusiano wa Muhimbili, Aminiel Aligaesha, alithibitisha kuchukuliwa kwa maiti ya mtoto huyo majira ya saa tano asubuhi baada ya kukabidhiwa kwa mlezi wake, Josephine Joel na maofisa wapelelezi wawili kutoka  Morogoro.
 
“Maiti ya mtoto Nasra imechukuliwa, tulimkabidhi mama yake mlezi aliyekuja naye na maofisa upelelezi ambao walikabidhiwa ripoti ya uchunguzi.
 
“Siwezi kuzungumza ripoti hiyo ina nini kwa sababu hiyo iko kisheria zaidi (Medical Legal Report) kutokana na tukio lenyewe lilivyo… pia siwezi kuwapeleka kwa daktari aliyefanya uchunguzi wa mwili wa mtoto huyo kwa sababu sheria haimruhusu kuzungumza,” alisema Aligaesha.
 
Mwandishi alimtafuta bila mafanikio daktari aliyeufanya uchunguzi mwili wa Nasra aliyefahamika kwa jina moja la Mwakyoma, hata ilipopigwa simu yake ya kiganjani iliita bila kupokelewa.
 
Hata hivyo mmoja wa madaktari waliokuwa wakimtibu Nasra ambaye hakutaka kutaja jina lake siku hiyo kwa kuwa siyo daktari wa zamu, alisema mtoto huyo amefariki akiwa kwenye mashine ya oksijeni iliyokuwa ikimsaidia kupumua.
 
“Mtoto Nasra alipofikishwa na kufanyiwa vipimo vya awali tulibaini ana utapiamlo, tukamuanzishia chakula na dawa, tuliendelea na vipimo akasema anaumia kifuani na kiuno, tukampima na kubaini ana nemonia wakati huo akashindwa kupumua tukamwekea mashine ya oksijeni,” alisema.
 
Katika hatua nyingine, baba mzazi wa mtoto huyo, Rashid Mvungi, alisema amekubaliana na uamuzi wa serikali wa kumzika mtoto wake.
 
Mvungi ambaye jana alionekana katika jengo la kuhifadhia maiti hospitalini hapo akiwa na ndugu zake wanne, alisema alipewa usafiri kwenda Dar es Salaam kuchukua maiti ya mtoto wake.
 
Hata hivyo baada ya gari lililobeba maiti ya mtoto wake kuondoka, nao waliingia katika gari aina ya Land Cruiser mali ya Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro na kuondoka.
 
Mtoto Nasra alifichuliwa Mei 21 mwaka huu na majirani ambao walimweleza Ofisa Mtendaji wa Kata ya Kiwanja cha Ndege, Dia Zongo kuwa alikuwa amefichwa katika boksi na mwanamke aliyetambuliwa kwa jina la Mariamu Said mkazi wa kata hiyo mkoani Morogoro.
 
Majirani hao walimweleza Zongo kuwa Nasra alifichwa ndani ya boksi tangu akiwa na miezi tisa mwaka 2009 na kwamba alikuwa hafanyiwi usafi wala kutolewa nje.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger