Friday 27 June 2014

WABUNGE WANUKA RUSHWA-DODOMA

...
INNOCENT-THE BLOGGER-BOY
bunge2 c927e

WAKATI muswada wa kupunguza misamaha ya kodi unatarajia kujadiliwa wakati wowote, kuna hofu kwamba baadhi ya wabunge wamehongwa na wafanyabiashara waliopiga kambi mjini hapa ili kuukwamisha.

Kuenea kwa taarifa za kuhongwa kwa wabunge, zimemfanya Spika wa Bunge, Anne Makinda, kuiita bungeni Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ili kuchunguza tuhuma hizo.
Taarifa za kuwapo kwa wafanyabiashara hao zilianza kuzagaa tangu wiki iliyopita wakati wabunge wakichangia bajeti ya serikali kwa mwaka 2014/2015 inayofikia sh trilioni 19.2 ambapo idadi kubwa ya wabunge waliunga mkono uamuzi wa serikali wa kutaka kufuta misamaha ya kodi isiyo na tija kwa taifa.
Katika mijadala ya wabunge ikiwemo taarifa ya Kamati ya Bajeti, ilikuwa ikilalamikia misamaha ya kodi ambayo kwa mwaka 2012/2013 ilikuwa sh trilioni 1.5 na hadi Aprili mwaka huu ilifikia sh trilioni 1.4.
Tanzania Daima ilidokezwa kuwa baadhi ya wabunge, wakiwemo wa Kamati ya Bajeti wamegawanyika katika makundi mawili ambapo moja linataka isifutwe kwa madai itawakimbiza wawekezaji na jingine linataka ifutwe ili taifa liwe na mapato ya kutosha.
Katika mijadala hiyo, Kamati ya Bajeti ilibainisha kuwa bajeti ya mwaka 2013/2014 ilikuwa na nakisi ya sh trilioni 2, hivyo kushauri kama serikali itafuta misamaha isiyo na tija itachangia kuimarisha mapato yake.
Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum, juzi alisema yupo tayari kwa mapambano na wabunge waliodhamiria kukwamisha muswada huo kwakuwa amesikia kuna waliojipanga kuuzuia ili kuwanufaisha wafanyabiashara.
Mkuya alisema anashangazwa na harakati hizo za wabunge ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakiilaumu serikali, kwamba inapoteza fedha nyingi katika misamaha ya kodi isiyo na tija kwa taifa.
"Mimi nitawashangaa sana wabunge mtakaopinga muswada huu wakati ndio nyinyi mnaotaka maji, umeme barabara, hospitali katika majimbo yenu... tumesikia kuna watu wanapita huko, lakini nataka niwahakikishie nimejipanga kikamilifu," alisema.
Akizungumza na Tanzania Daima jana katika viwanja vya Bunge, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, alisema wabunge wanapaswa kuwa kitu kimoja katika kuunga mkono muswada huo kwakuwa ndio utakaosaidia serikali kuongeza mapato yake.
Mwigulu alisema wanashangazwa na misimamo iliyoanza kuonyeshwa na baadhi ya wabunge kutaka kukwamisha muswada huo wakati wao ndio waliokuwa vinara wa kutaka misamaha hiyo ifutwe.
"Kweli hata sisi tunashangaa wenzetu wamepatwa na kitu gani kiasi cha kuanza kuonyesha dalili za kutukwamisha, sisi tulidhani wenyewe ndio wangekuwa mstari wa mbele kushangilia jambo hili, tunawaomba wasikubali ushawishi wa wafanyabiashara wanaoranda randa hapa Dodoma.
"Tunajua wafanyabiashara hawataki misamaha hii ifutwe, hivyo watafanya kila jambo isifutwe, wabunge wawe makini sana na ushawishi wanaopewa na watu hao..., nchi yetu inahitaji maendeleo, bila kodi hakuna maendeleo," alisema.
Spika Makinda azungumza
Akizungumza na Tanzaia Daima, Spika wa Bunge, Makinda, alisema wabunge kukutana na wafanyabiashara kuzungumzia muswada huo si dhambi kwakuwa wanapata fursa ya kuelewa zaidi hatua itakayowasaidia kwenye maamuzi.
Alisema ushawishi unaofanywa na wafanyabiashara si tatizo kwa sababu jambo lolote zuri linaanza na ushawishi ambao huwawezesha wahusika kujua baya na zuri la lile wanalotaka kulifanya.
"Hata sisi humu bungeni tunashawishiana juu ya jambo fulani, lakini mwisho wa siku kila mmoja ana uamuzi wake ambao unapaswa uangalie masilahi ya taifa kuliko binafsi.
"Kila siku ninapinga wabunge kufanya uamuzi kwa kufuata maslahi ya kundi fulani la watu, bali ninataka wafanye kwa kuzingatia maslahi ya umma, sasa kama wafanyabiashara wanawashawishi wabunge waukwamishe muswada na wao wakafanya hivyo, hilo litakuwa jambo la kusikitisha sana," alisema.
Spika Makinda, alisema anaikaribisha Takukuru kufanya uchunguzi wa tuhuma za wabunge kuhongwa na wafanyabiashara ili wakwamishe muswada wa kufuta misamaha ya kodi.
"Kama wabunge wenzetu wanapewa rushwa ili wakwamishe muswada huu, naomba Takukuru waje walifanyie kazi jambo hili, tunahitaji maendeleo kwa taifa ambayo yanapatikana kutokana na kodi zinazolipwa," alisema.
CHANZO TANZANIA DAIMA
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger