Sunday 22 June 2014

Mapendekezo ya Kamati za Bunge Maalumu yanayodhoofisha Muungano – 2

...
INNOCENT-THE BLOGGER-BOY

Makala haya ni mwendelezo wa makala yaliyoanza wiki iliyopita. Madhumuni ya makala hizi ni kupitia kamati zote za Bunge Maalumu kiuchambuzi ili kubaini mapendekezo ambayo yanadhoofisha Muungano. Aidha, uchambuzi huu utawawezesha wadau wote katika mchakato wa kuandika Katiba Mpya ya Tanzania ikiwamo wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kuwa na utambuzi wa kina kuhusu Rasimu ya Katiba Mpya.
Kamati namba 1 katika ukurasa wake wa 8 inasema “kiutawala na kimamlaka” Serikali ya Muungano kama ilivyopendekezwa katika Rasimu inatenganishwa na wananchi kwa sababu haihusiki na mambo yanayowagusa wananchi moja kwa moja. Hoja hii ya Kamati haina mashiko na haiakisi uhalisia sasa wa namna Serikali inaevyoenenda kiutawala na kimamlaka, lakini pia huu sio uhalisia wa yaliyomo katika Rasimu ya Katiba Mpya Toleo la Pili.
Katika Muundo wa sasa Rais wa Jamhuri ya Muungano hana uhusiano wa moja kwa moja na raia wa Tanzania waishio Tanzania Zanzibar hasa katika masuala ya maendeleo ambayo ndiyo yanayowagusa watu wa kawaida moja kwa moja. Mambo haya si ya Muungano Kikatiba. Mfano mzuri ni sekta zote muhimu si mambo ya Muungano kivitendo, sekta hizi ni pamoja na Kilimo, Afya, Uchukuzi, Miundombinu na Elimu.
Aidha, kwa kuzingatia marekebisho ya Katiba ambayo yameshafanyika hasa kwa Katiba ya Zanzibar na mabadiliko yasiyo rasmi katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano. Uhalisia ni kwamba, Rais wa Jamhuri ya Muungano hushughulikia mambo ya Maendeleo Kikatiba kwa Watanzania waishio Tanzania Bara au Tanganyika pekee. Kitendo hiki kinawatenga Watanzania waishio Zanzibar na kinamwondolea Rais wa Jamhuri ya Muungano wajibu wa moja kwa moja wa kuwahudumia Watanzania kutoka pande zote mbili za Muungano kwa usawa.
Rasimu inapendekeza Sura nzima ya Pili inayozungumzia Malengo Makuu na Misingi ya Mwelekeo Shughuli wa Serikali na Sera za Kitaifa. Hapa ndiyo tunazungumzia Dira ya Maendeleo ya Taifa ambayo Mamlaka zote Tatu zinapaswa kuitekeleza kupitia Mambo ya Muungano (rejea Ibara ya 63) na Mambo yasiyo ya Muungano (rejea Ibara ya 64, 65 na hasa Ibara ya 111[1][b]).
Unapowianisha sera na sheria kwa mambo yasiyo ya Muungano chini ya usimamizi wa Jamhuri ya Muungano, ndiyo dhana inayostawisha usawa, haki, ushiriki wa moja kwa moja, mshikamano, kusaidiana na kupelekea maisha bora kwa kila Mtanzania kokote anapoishi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, iwe ni Tunduru au ni Tumbatu.
Kitendo hiki ndio ambacho hasa Rasimu ya Katiba inapendekeza katika nchi yetu, kitendo hiki sio tu kitaimarisha Muungano wetu na kutatua kero na changamoto za wananchi bali ndio kitendo kitakachoimarisha Jamhuri ya Muungano ikiwa na umoja wa kitaifa na usalama.
Kamati inaendelea katika taarifa yake ukurasa wa 9 kwa kuweka pendekezo la eneo la Jamhuri ya Muungano linalosomeka eneo la Jamhuri ya Muungano ni eneo lote laTanzania Bara na eneo lote la Zanzibar na linajumuisha sehemu zake zote za bahari, maziwa, mito na maeneo mengine yatakayoongezwa.
Ili kulielewa pungufu la pendekezo hili yapasa kuelewa mambo kadhaa, Kwanza ni usanifu na uandishi wa Katiba na namna Rasimu ilivyoandikwa. Pili ni uwepo wa Mikataba ya Kimataifa inayosimamia mipaka ya nchi na hapa nitafafanua Mikataba ya Kimataifa ambayo inasimamia mipaka ya Tanzania katika ardhi (iwe tambarare, milima, vilima au mabonde) na kwenye maji (iwe mito, maziwa au bahari sehemu ya nchi pamoja bahari kuu) na tatu ni mifano ya nchi nyingine.
Usanifu na uandishi wa Katiba ni stadi na ni muundo wa namna Katiba inavyoandikwa na kupangwa kwa maana ya sura, sehemu na vifungu. Uandishi na usanifu unazingatia kuhakikisha vifungu vinafahamiana, vinasomeka pamoja, vinashirikiana na kwa namna yoyote havigongani. Katiba katika usanifu yaweza kuchukua muundo ambao umejikita katika kueleza misingi pekee au kuweka misingi pamoja na masharti yanayojifafanua au Katiba ikaandikwa ikiwa na masharti yanayojifafanua kwa kina kwa kiingereza ‘prescriptive.’
Usanifu wa Rasimu ya Katiba Mpya Toleo la Pili umezingatia muundo unaojumuisha Misingi na Masharti yanayojifafanua kwa pamoja. Muundo huu ndiyo uliotumika kuandika Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya 1977 Toleo la Mwaka 2005. Ili kuielewa Rasimu ni lazima usome masharti yake kwa pamoja au ‘in tanderm’ kwa lugha ya Kiingereza. Nachelea kusema kama uandishi wa pendekezo la Kamati ulizingatia uhalisia huu.
Ukitaka kuielewa Ibara ya 2 ya Rasimu inayozungumzia eneo la Jamhuri ya Muungano (kama Msingi) ni lazima uisome na Ibara ya 49 inayohusu pamoja na mambo mengine, wajibu wa raia kuilinda Jamhuri ya Muungano, Ibara ya 51 inayozungumzia ulinzi wa mali ya umma, hii ikijumuisha eneo letu la ardhi kama Nchi na Taifa na Ibara ya 235(2) inayozungumzia ulinzi wa mipaka ya Jamhuri ya Muungano. Utagundua hasa Ibara 235(2) inaweka masharti yanayotoa ufafanuzi wa Ibara ya 2 katika muktadha wa ulinzi wa eneo la Jamhuri ya Muungano ikijumuisha ardhi, anga na bahari kuu. Mito na maziwa ni sehemu ya pande la ardhi.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger