Thursday 26 June 2014

NGUMI BUNGENI:JAJI WEREMA AMFANANISHA MBUNGE KAFULILA NA TUMBILI TAFRANI YAIBUKA, MAWAZIRI WAINGILIA KATI

...
INNOCENT-THE BLOGGER-BOY


Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, ameteleza ulimi tena na mara hii amejikuta akimuita Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi) tumbili.

Kabla ya kutoa kauli hiyo, Werema alikuwa akitoa ufafanuzi wa mwongozo ulioombwa na Kafulila, kuhusu fedha zilizokuwa katika akaunti ya Escrow iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ambazo zimelipwa kwa kampuni ya PAP, inayomiliki mitambo ya kampuni ya umeme ya Independent Power Tanzania Limited(IPTL).
Werema alisema fedha hizo si za Serikali, kama inavyodaiwa na Kafulila, kwa kuwa fedha za Serikali, hazikai katika akaunti hiyo.
Alifafanua kuwa taarifa zinazotolewa, zinapotosha umma kuwa serikali imetoa fedha kuilipa IPTL, wakati ukweli ni kuwa fedha hizo ziliwekwa katika akaunti hiyo, kutokana na misuguano baina ya wanahisa wawili, waliokuwa wamiliki wa IPTL.
Werema alibainisha kuwa mmoja wa wanahisa hao, alikuwa akitaka IPTL ifilisiwe, huku mwingine akipinga jambo hilo mpaka walipouza hisa zao na kumaliza mgogoro huo, ambapo Mahakama iliruhusu mali za kampuni hizo,  apewe mwanahisa mpya, PAP.
Werema alisema kuna watu walileta bungeni  vipeperushi, wakidai ni ushahidi kuhusu utoaji wa fedha hizo za akaunti ya Escrow na kuhusisha na rushwa.
"Kafulila ni miongoni mwa  wanaoeneza taarifa potofu…kama ni tuhuma au kuna rushwa, itakuja kujulikana, tusubiri uchunguzi wa vyombo husika,”alisema.
Wakati akizungumza, Werema alitumia mfano wa kabila la Wanyankole, aliosema kuwa wana usemi unaosema kwamba 'Tumbili hawezi kuamua kesi ya msituni'.
Kabla ya kufafanua maana ya msemo huo, Kafulila bila kuwasha kipaza sauti, alikuwa akipiga kelele kumuita Werema kuwa ni mtuhumiwa, hivyo atangaze maslahi yake.
“Naomba nisikilize, hata kama ni mtuhumiwa, nina fursa ya kusikilizwa …nisikilize wewe tumbili,” alijikuta akisema Werema.
Baada ya kusema hivyo, Kafulila hakukubali ;na yeye bila kuwasha kipaza sauti, alisema: “Wewe (Werema) ni mwizi tu.”
Kutokana na hali hiyo, Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Azan 'Zungu' alimuomba Jaji Werema, kukaa chini ili atoe ufafanuzi, huku Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema) na Kafulila wakitaka kuzungumza.
Zungu alisema kwa kuwa Bunge, lilishaamua kuwa suala hilo, lipelekwe Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) na kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ni vyema kama Kafulila ana ushahidi wowote, apeleke huko.
Baada ya kutoa mwongozo huo, ambao ulisitisha malumbano, Mwenyekiti Zungu alisitisha shughuli za Bunge mpaka jioni na kuondoka, huku akisindikizwa na makatibu wa Bunge na wapambe kama kawaida.
Hatua ya Mwenyekiti wa Bunge kuondoka katika ukumbi, baada ya kusitisha shughuli za Bunge, ilimpa fursa Jaji Werema kuweka sawa makabrasha yake na kutoka katika kiti chake, ambapo alionekana kama vile anakwenda kumkabili Kafulila.
Wakati hilo likitokea, Mbunge wa Maswa Mashariki, Sylvester
Kasulumbayi (Chadema), alihama katika kiti chake na kukimbilia alipokuwa amekaa Kafulila.
Katika hali isiyokuwa ya kawaida, baadhi ya mawaziri  walimzunguka Jaji Werema, kabla hajamfikia Kafulila na Kasulumbayi.
Mawaziri hao ni Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu, Stephen Wassira, Waziri wa Sheria na Katiba, Dk Asha Rose Migiro na Naibu Waziri wa Afrika Mashariki, Dk Abdullah Juma Abdullah Saadalla.
  
Nje ya Bunge, Kafulila na Mnyika waliitisha mkutano na waandishi wa habari, ambapo walidai kuwa na ushahidi wa kutuhumu baadhi ya mawaziri, kusema uongo bungeni kuhusu fedha hizo za Escrow.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger