Saturday 28 June 2014

DIAMOND PLATNUMZZ KATIKA BET AWARDS NYINGINE TENA

...
INNOCENT-THE BLOGGER-BOY


Nasibu Abdul ‘Diamond Plutnumz’.
UMEKUCHA! Unaweza kusema kwa maana nyingine wakati wasanii kutoka Afrika watakapokuwa pamoja kwenye Ukumbi wa Nokia Theatre uliopo Los Angeles, Marekani katika sherehe za utoaji tuzo za BET 2014 kesho Juni 29.
Macho na masikio yote yameelekezwa kwa mtu mmoja kutoka Tanzania ambaye ni Nasibu Abdul ‘Diamond Plutnumz’.

Kupitia wimbo wa My Number One (Remix), aliomshirikisha staa kutoka pande za Nigeria, Davido, ndiyo uliompandisha chati za juu mpaka kufikia kujulikana kimataifa sambamba na kuingizwa katika tuzo mbalimbali za heshima.
Wapo wanaofurahia mafanikio yake na wengine kuchukia na kuona kama anapendelewa.
Katika makala haya yanachambua safari nzima za tuzo ambazo ameshashiriki na anazoendelea kushiriki kwa sasa;
Awashangaza Watanzania
Aliivunja rekodi iliyokuwa ikishikiliwa na mwanamuziki Abass Hamis Kinzasa ‘20%’,  ya mwaka 2011 ambayo alijinyakulia tuzo tano kwa mpigo zilizotambulika kama Kilimanjaro Music Awards 2011.
Katika tuzo za Kilimanjaro za mwaka 2014 zilizofanyika Mlimani City jijini Dar, Diamond aliondoka shujaa kwa kujizolea tuzo saba kwa mpigo na kuweka rekodi ya aina yake huku maswali mengi yakibaki midomoni mwa watu na hata wengine wakidhani amebebwa na hakustahili kupewa tuzo hizo zote.
Atemwa tuzo za MTV MAMA 2014
Mpaka Diamond anaelekea Afrika Kusini Juni 7 mwaka huu, alionekana kama msanii anayeongoza kwa kupigiwa kura nyingi na mashabiki akiwa na asilimia zaidi ya 60. Watanzania wengi walijua ataibuka kidedea.
Wakati wa ufunguzi wa tuzo hizo alianza kwa kufanya shoo ya nguvu akiwa sambamba na mwanamuziki kutoka Nigeria, Davido. Walilivaa jukwaa na wimbo wa My Number One Remix.
Hata wale ambao hawakujua lugha ya Kiswahili aliyokuwa akiimba Diamond katika wimbo huo walionekana kumfurahia kwa kucheza naye pamoja.
Kilichokuja kufanyika wakati wa utoaji wa tuzo hizo, Diamond hakuambulia kitu chochote. Tuzo zilimpita machoni na kukimbilia kwa wasanii kama Davido, Tiwa Savage, Uhuru pamoja na Mafikizolo.

Atatoka katika tuzo za BET 2014?
Habari kila kona ni siku ya kesho Juni 29, katika utoaji tuzo za BET 2014 ambapo Diamond ameingia katika kategori ya Mwanamuziki Bora wa Kimataifa kutoka Afrika akiwa sambamba na Sarkodie (Ghana), Mafikizolo (Afrika Kusini), Davido (Nigeria), Toofan (Togo) na Tiwa Savage (Nigeria) ambao wote kwa pamoja wameshaning’iniza kwapani tuzo za MTV Afrika 2014 na za BET 2012 kasoro Diamond kutoka Tanzania.
Abaniwa kupafomu
Swali gumu la kujiuliza ni jinsi mpangilio mzima uliopangwa na waandaaji wa tuzo za BET 2014 zitakazofanyika kesho.
Wakati wale waandaaji wa MTV Afrika 2014 walimpa Diamond nafasi ya kupafomu wimbo wake kwa kushirikiana na Davido, mambo yamekuwa tofauti kwa BET 2014.
Wamewakusanya wasanii wengi kutoka Nigeria mbaya zaidi ni wale wanaoshirikiana naye katika kugombea tuzo hizo ambapo kesho watapanda jukwaani kwa pamoja na kuimba wimbo maalum unaohusu Afrika.
Wasanii hao ni pamoja na Sarkodie kutoka Ghana, Mafikizolo kutoka Afrika Kusini, Tiwa Savage na Davido wote kutoka Nigeria.

Abakiza tuzo mbili tu
Bado anayo nafasi kubwa ya kusonga mbele na kugombea tuzo mbalimbali za kimataifa hata kama katika tuzo za BET atazikosa kesho. Mpaka sasa amebakiza tuzo mbili ambazo ni AFRIMMA 2014 na zile za KORA Africa 2014.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger