FAMILIA
tano za walimu wa shule ya sekondari Shishani Kata ya Migato
Halmashauri ya Itilima Mkoani Simiyu, zinaishi jengo la utawala tangu
mwaka 2013.
Hali hiyo inatokana na ukosefu wa nyumba za walimu ambapo sasa shughuli za utawala shuleni hapo zinafanyika chini ya mti.
Mwalimu
Mkuu wa shule hiyo, Tito Kwilasa alisema hayo jana wakati akizungumza
na waandishi wa habari, waliofika shuleni hapo kwa ajili ya kikao cha
maendeleo ya kata kilichojadili changamoto mbalimbali zilizopo.
Kwilasa alibainisha kuwa shule hiyo yenye wanafunzi 160, iliyoanzishwa mwaka 2007 ina uhaba mkubwa wa nyumba za walimu.
Nyumba
za walimu zilizopo shuleni hapo ni mbili wakati kuna walimu 15
walioajiriwa, ambapo wanawake ni watatu na wanaume 12. Kwa sasa walimu
hao wanaishi jengo la utawala, ambapo shule ina madarasa manne na
maabara iliyofikia usawa wa madirisha.
‘’Kipindi
cha mvua za masika inabidi kutoa darasa moja likachanganywe na lingine
ili walimu tukakae darasani na kufanya shughuli za utawala huku
wanafunzi hao wakikosa masomo,” alisema.
Alisema
kuwa kipindi cha nyuma walimu walikuwa wachache, hivyo walibanana
katika nyumba hizo mbili. Mwaka 2013 walimu waliongezeka, hivyo
waligeuza jengo la utawala kuwa nyumba ya kuishi. Mwalimu mmoja alisema
ni kero kubwa kwa familia hizo kuishi jengo la utawala ambalo pia halina
vyoo.
Diwani
wa Kata hiyo, Mbuga Ntobi alieleza kuwa watahakikisha walimu
wanajengewa nyumba ili waishi katika mazingira ya ufundishaji.
Mkurugenzi
wa Halmashauri ya Itilima, Kelisa Wambura alithibitisha kuwepo kwa hali
hiyo. Alisema halmashauri imepanga kwenye bajeti ya 2016/17 kupunguza
uhaba wa nyumba za walimu, hasa shule ya sekondari Shishani.
0 comments:
Post a Comment