Tangu
wabunge wa upinzani waanze kususa vikao vinavyoongozwa na Naibu Spika,
Dk Tulia Ackson, kiongozi huyo wa Bunge ameamua ‘kukomaa’ na kiti hicho,
hatua inayosababisha wapinzani wasipate fursa ya kutia mguu bungeni.
Kwa
kawaida, Spika wa Bunge, Job Ndugai au naibu wake wanapokuwa na
shughuli nyingine, huachia kiti hicho kwa wenyeviti watatu wa Bunge
kuendesha vikao, lakini safari hii Dk Tulia amekuwa akiingia kila siku
asubuhi na jioni.
Mei
31, mwaka huu wabunge wote wa upinzani walianza kususa vikao
vinavyoendeshwa na kiongozi huyo kwa madai ya kutokuwa na imani naye,
hasa baada ya kuzuia hoja ya kufukuzwa kwa wanafunzi 7,802 katika chuo
cha Udom.
Hoja
hiyo iliwasilishwa na Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari
lakini Dk Tulia alisema haikuwa na umuhimu kwa wakati huo, jambo
lililozua tafrani baina ya kiongozi huyo na wabunge wote wa upinzani.
Kutokana
na hali hiyo, wabunge hao walipitisha azimio la kususa vikao
vinavyoendeshwa na kiongozi huyo na tangu siku hiyo, kila anapoingia
bungeni kuongoza kikao wamekuwa wakitoka ukumbini.
Spika
wa Bunge, Job Ndugai ambaye kwa sasa yuko nchini India kwa matibabu,
amekuwa akisaidiwa na Dk Tulia pamoja na wenyeviti watatu wa Bunge ambao
ni Mbunge wa Ilala (CCM), Mussa Azzan Zungu, Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge na Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Najma Giga.
Tangu
wapinzani waamue kususa vikao vinavyoendeshwa na Dk Tulia, kiongozi
huyo wa Bunge amekuwa akiendelea kuongoza vikao na kuwafanya wapinzani
kila siku kutoka katika ukumbi huo.
Hata
hivyo Dk Tulia alieleza bungeni kuwa kama kuna mbunge yeyote ambaye
anahisi hatendewi haki, kanuni za Bunge zinatoa nafasi namna ya
kuwasilisha malalamiko yake.
Kutokana
na hali hiyo, wabunge wa upinzani kupitia kwa Mbunge wa Simanjiro
(Chadema), James Millya waliwasilisha hoja kwa Spika ya kuazimia
kumng’oa madarakani Naibu Spika.
Hoja
sita za Millya zilipokelewa na ofisi ya Katibu wa Bunge kwa niaba ya
Spika ambaye yuko nje, zikibainisha kuwa wabunge hao hawana tatizo na
kiti bali Dk Tulia.
Spika
Ndugai atatakiwa kuwasilisha barua hiyo ya kusudio la kumng’oa Dk
Tulia katika Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kwa ajili ya
kushughulikiwa.
Pamoja
na suala lake kupelekwa kwenye kamati hiyo, Dk Tulia alitoa mwongozo
ulioombwa na Mbunge wa Nkasi Kaskazini(CCM), Ally Keissy kuhusu posho
kwa wabunge wote wa upinzani wanaoingia na kutoka nje bila kufanya kazi.
Alisema wabunge ambao hawashiriki vikao vya Bunge hawatalipwa posho.
0 comments:
Post a Comment